May 24, 2024 07:48 UTC
  • Jeshi la Iran latoa ripoti ya awali kuhusu ajali ya helikopta iliyopelekea kufa shahidi Raisi

Kamandi Kuu ya Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema uchunguzi wao wa awali umebaini kuwa, hakuna kitu chochote kisichokuwa cha kawaida kinachoweza kuhusishwa na ajali ya helikopta iliyotokea Jumapili iliyopita katika mkoa wa Azarbaijan Mashariki, kaskazini magharibi mwa nchi.

Ripoti ya uchunguzi huo wa awali inasema kuwa, helikopta hiyo ilifuata ratiba na njia iliyokuwa imepangiwa tangu mwanzo, na wala haikukengeuka. 

Kamandi ya Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeeleza kuwa: Hakuna alama zozote za kuashiria kuwa helikopta hiyo ilitunguliwa au kushambuliwa.

Imeeleza kuwa, mawasiliano yaliyofanyika kabla ya tukio hilo la Jumapili baina ya ndege (helikopta) na maafisa wanaodhibiti safari za anga yanaonesha hakuna jambo lolote la kuibua shaka na kuongeza kuwa, taifa la Iran litafahamishwa kuhusu maelezo zaidi juu ya ajali hiyo.  

Helikopta iliyokuwa imembeba Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jumapili jioni Mei 19, 2024 ilipata ajali ilipokuwa ikirejea kutoka kwenye hafla ya ufunguzi wa bwawa la Qiz Qalasi kwenye mpaka wa pamoja wa Iran na Jamhuri ya Azerbaijan.

Wakati helikopta hiyo ilipokuwa inaelekea mji wa Tabriz, ilianguka katika eneo la Varzghan mkoani Azarbaijan Mashariki, kaskazini-magharibi mwa Iran. Ndani yake walikuwemo pia Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje, Imam wa Ijumaa wa Tabriz, Gavana wa Azarbaijan Mashariki na watu wengine; na wote pamoja wakaifika hadhi tukufu ya kufa shahidi.

Marehemu Sayyid Raisi alizikwa jana usiku katika Haram tukufu ya Imam Ridha AS katika mji mtakatifu wa Mashhad ulioko kaskazini mwa Iran, huku mwili wa Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje ukizikwa hiyo hiyo jana katika Haram ya Shah Abdol-Adhim katika mji wa Shahre-Rey, kusini mwa Tehran.

Tags