Jan 29, 2023 13:19 UTC
  • Ajali mbaya ya barabarani yaua watu 40 nchini  Pakistan

Kwa akali watu 40 wamepoteza maisha katika ajali mbaya ya basi iliyotokea huko kusini magharibi mwa Pakistan.

Hamza Anjum, afisa wa ngazi ya juu wa serikali katika wilaya ya Lasbela mkoani Balochistan, kusini magharibi mwa Pakistan amesema ajali hiyo iliyohusisha basi la abiria imetokea mapema leo Jumapili.

Amesema basi hilo lilipoteza muelekeo na kuanguka kutoka kwenye daraja, kabla ya kuripuka. Amesema maiti za abiria hao zimeungua kiasi cha kutoweza kutambulika.

Duru za habari zinaarifu kuwa, basi hilo lilisafiri usiku kucha likitokea Quetta, makao makuu ya mkoa wa Balochistan, likielekea katika mji wa badari wa Karachi, kusini mwa nchi. Anjum amesema inasadikika kuwa, yumkini basi hilo liliacha njia na kubingiria darajani baada ya dereva kusinzia.

Katika hatua nyingine, watoto wasiopungua kumi wameaga dunia leo Jumapili katika ajali ya boti iliyotokea kaskazini magharibi mwa Pakistan. 

Boti yazama na kusababisha maafa Pakistan

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, hatima ya watoto wengine wanane haijulikani, na kwamba wengine saba wamelazwa hospitalini katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kohat, Mahmood Aslam amesema takriban wanafunzi 50 kutoka shule moja ya kidini walikuwa kwenye boti hiyo iliyozama katika Ziwa Tanda, wakienda katika safari ya kimasomo. Wengine 25 wamenusurika kwenye ajali hiyo.

Tags