Ulimwengu wa Spoti, Jan 5
https://parstoday.ir/sw/news/event-i135136-ulimwengu_wa_spoti_jan_5
Natumai huna neno hapo ulipo mskilizaji mpenzi. Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu yaliyoshuhudiwa viwanjani ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa.
(last modified 2026-01-06T09:08:46+00:00 )
Jan 05, 2026 08:04 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Jan 5

Natumai huna neno hapo ulipo mskilizaji mpenzi. Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu yaliyoshuhudiwa viwanjani ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa.

Iran yawatuza wachezaji waliokataa kuchuana na Wazayuni

Katika hafla iliyofanyika hapa mjini Tehran, wanamichezo ambao katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita walikataa kushindana dhidi ya wawakilishi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walitunukiwa tuzo za heshima, kutokana na kitendo chao hicho kinachoashiria mshikamano na wananchi madhulumu wa Palestina. Sherehe hiyo iliwaleta pamoja maafisa wakuu wa michezo, wakuu wa mashirikisho, wanamichezo, na familia za mashahidi, ambapo washiriki walisisitiza uungaji mkono thabiti wa Iran kwa Palestina kupitia kile maafisa walichoelezea kama uanamichezo wenye misingi ya utu. Kukataa wanamichezo hao wa Iran kushindana dhidi ya wawakilishi wa utawala ghasibu wa Israel kunadhihirisha upinzani mkubwa kwa sera za Israel dhidi ya watu wa Palestina na kunaonyesha dhamira thabiti ya Jamhuri ya Kiislamu ya kupinga ukandamizaji.

Mohammad Shervin Asbaghian, Naibu Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran

 

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Sayyid Mohammad Shervin Asbaghian, Naibu Waziri wa Michezo na Vijana kwa Maendeleo ya Ubingwa na Michezo ya Kitaalam, pamoja na wakuu kadhaa wa shirikisho la michezo, wanariadha, na wanamichezo wakongwe. Amezipongeza timu za Iran kwa kupiga saluti katika mashindano ya kieneo na kimataifa, ikiwa ni salamu rasmi ya kijeshi, wakionyesha kuvienzi vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu vilivyopambana kishujaa dhidi ya utawaa wa Kizayuni katika vita vya siku 12 mwezi Juni mwaka uliomalizika wa 2025. Naibu Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran amesema: Leo hii, wanamichezo wetu mashupavu, walikuwa na nafasi muhimu katika vita vya siku 12. Saluti ya kijeshi iliyopigwa na wanamichezo wetu azizi hususan timu ya taifa ya vijana ya voliboli ya Iran, ilikuwa tafakuri kwa utambulisho wetu wa kidini, iliyokuja wakati hasasi wa vita vya siku 12, ambapo mashambulizi ya vikosi vya NATO, utawala wa kibeberu na utawala wa Kizayuni, yaliitikisa dunia.

Wanamichezo 20 kutoka fani mbalimbali za michezo walituzwa wakati wa hafla hiyo. Maafisa wa Iran walioshiriki wamepongeza uamuzi wa wanariadha na wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kutoshindana dhidi ya wapinzani wa Israel, na kuweka michezo ndani ya muktadha mpana wa kimaadili na kisheria. Mehdi Mirjalili, Mkuu wa Shirika la Kuhamasisha Wanariadha la Iran, kwa upande wake amesema: "Mashujaa na wapiganaji wa kweli ni wale ambao wamekataa kushindana dhidi ya wanamichezo wa utawala wa Kizayuni. Leo, baba ya shahidi Parsa Mansour, mtoto wake wa pekee, ambaye aliuawa shahidi katika vita vya siku kumi na mbili, ameungana nasi katika sherehe hii ya heshima. Tuna deni kubwa la shukrani kwenu, mashujaa wetu wa daima."

Mieleka: Mirzapour bingwa wa nchini Iran

Ahmad Mirzapour ameshinda taji la Mieleka ya 2025 ya Iran ya Pahlevani siku ya Ijumaa. Alimshinda Mostafa Taghani katika safu ya wanamieleka wenye uzani wa kilo zaidi ya 100. Mashindano ya Mieleka ya Pahlevani hufanyika kila mwaka nchini Iran, kwa kuwachuanisha wanamieleka bingwa kutoka kote nchini.

Ahmad Mirzapour, mshindi wa Pahlevan 2025

 

Ingawaje shindano hili lina asili ya jadi, lakini hii leo limefanywa ya kisasi baada ya kufanyiwa marekebisho tangu 1944. Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) lilisajili mashindano ya Pahlevani na Zourkhaneh katika orodha ya Turathi za Utamaduni wa Kale mwaka wa 2014.

Futsal: Wairani wateuliwa kuwania tuzo

Wanamichezo wanne wa mchezo wa futsal wa Iran wameteuliwa kuwania duru ya 26 ya Tuzo za Dunia za Futsal za kila mwaka, zinazotolewa na shirikisho la kusimamia mchezo huo duniani. Kipa wa timu ya taifa ya Iran ya futsal ya wanaume Bagher Mohammadi ameorodheshwa kuwania tuzo ya Kipa Bora kwa Wanaume Duniani. Atachuana na Dennis Vasconcelos Cavalcanti (Brazil), Juan Cruz Freijo Riveras (Argentina), Leonardo “Léo” Gugiel (Brazil), Matheus Marcos de Lima Assunção (Brazil), na Mathías Gabriel Fernández Krigeris (Uruguay). Kwa upande wa wanawake, Maral Torkaman ameteuliwa kuwania Mchezaji Bora Chipukizi kwa Wanawake Duniani 2025. Wengine wanaochuana ni Jasmine Demraoui (Morocco), Emylly Sofia de Figueredo Cabrera (Brazil), Greta Ghilardi (Italia), Merlin Yovhana Salcedo Ramos (Colombia), na Rikako Yamakawa (Japan). Nyota wa Iran, Hossein Tayebi pia ameorodheshwa kuwania Mchezaji Bora wa Wanaume Duniani 2025. Anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Bruno de Seixas Martins "Bruninho" (Brazil), Soufiane El Mesrar (Morocco), Marcel de Mendonça Marques (Brazil), Pablo Ramírez González (Uhispania), na Jean Wabrazili Pierto Guise na Pierto Guise.

 

Wakati huo huo, kocha mkuu wa timu ya taifa ya wanaume ya futsal ya Iran, Vahid Shamsaei ameteuliwa kuwania Tuzo ya Kocha Bora wa Timu ya Taifa ya Wanaume Duniani. Wapinzani wake ni pamoja na Hicham Dguig (Morocco), Blazej Korczynski (Poland), Oleksandr Kosenko (Ukraine), Marcos “Marquinhos” Xavier Andrade (Brazil), Matías Raúl Lucuix (Argentina), na Héctor Souto (Hispania), kocha mkuu wa Indonesia. Washindi wa tuzo hizo za kifahari watatangazwa Jumatano ijayo ya Januari 7.

Uadui wa US kwa wanamichezo wa Iran

Bingwa wa tenisi ya meza raia wa Iran, Amirhossein Hedayati amenyimwa viza na serikali ya Marekani kutokana na vikwazo vipya vya usafiri nchini humo, vinavyoathiri raia wa mataifa kadhaa. Kwa hatua hayo, Amirhossein Hedayati ambaye alishinda medali katika Michezo ya Asia ya Hangzhou na Michezo ya Mshikamano wa Kiislamu, atakosa fursa ya kushiriki mechi muhimu nchini Marekani msimu huu.

AFCON; Mibabe yaaga

Siku ya Jumapili, timu ya taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) ilishuka dimbani kuvaana na Morocco katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ikifahamu fika kuwa inawajihiwa na kibarua kigumu. Stars ilipambana kiume hata hivyo na kuwahemesha wenyeji, ambao hatimaye walivuna ushindi hafifu wa bao moja bila jibu. Bao pekee la Morocco lilifungwa kunako dakika ya 64 na Brahim Díaz, na kuwawezesha Waarab hao kusonga mbele hadi robo fainali  katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika. Kwa upande wa Tanzania, ni mara ya kwanza katika historia yake kufika hatua ya 16 bora ya michuano ya AFCON tangu kuanzishwa kwake. Refa aliyeongoza mchezo huo amejikuta kwenye lawama kali kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka, baada ya kudaiwa kushindwa kutafsiri vyema sheria za mchezo huo. Baadhi ya Watanzania wamesema Taifa Stars walinyimwa penati ya wazi kipindi cha pili cha mchezo huo, baada ya mchezaji wa Morocco kudaiwa kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari. Licha ya malalamiko kutoka kwa wachezaji wa Tanzania, refa aliendelea na mchezo bila hata kwenda kuangalia teknolojia ya VAR, jambo lililozua mjadala mkubwa uwanjani na mitandaoni.

 

Watanzania mitandoni wamemualika refa huyo kwenda Tanzania kidogo, wafanye mazungumzo ya faragha. Kabla ya hapo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikuwa ameizawadia Taifa Stars shilingi milioni 500 kufuatia kufanikiwa kufuzu hatua ya 16 bora katika michuano hiyo ya AFCON. Taarifa hiyo ilitolewa Jumamosi ya Januari 3 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, wakati akizungumza na wachezaji pamoja na benchi la ufundi la Taifa Stars kwa njia ya simu. Katika hatua nyingine, penati mbili alizookoa kipa wa Yanga, Djigui Diarra, zimemfanya apate Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi na kuiwezesha timu yake ya taifa ya Mali kuing’oa Tunisia na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya kibara. Mali wakiwa wachezaji 10 kwa dakika zaidi ya 70 baada ya Woyo Coulibaly kulishwa kadi nyekundu dakika ya 26, waliweza kumudu kumaliza mchezo kwa sare ya bao 1-1. Coulibaly alikumbana na adhabu hiyo baada ya kumpiga kiatu staa wa Tunisia, Hannibal Mejbri. Tunisia walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Firas Chaouat, kisha Yassine Meriah kuisawazishia Mali kwa mkaju wa penalti iliyotokana na mchezaji wa Tunisia ‘kuunawa’ mpira kwenye sanduku la hatari. Licha ya ubora wa Tunisia, Mali ilibaki imara na hatimaye kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 kwenye upigaji matuta.

 

 

Kwa ushindi huo, sasa Mali watasafiri hadi mjini Tangier kuifuata Senegal kwa mchezo wa robo fainali utakaochezwa Ijumaa ya wiki ijayo. Senegal ilianza kwa kufungwa mapema kipindi cha kwanza katika mchezo dhidi ya Sudan. Hata hivyo, kabla ya mapumziko walifanikiwa kusawazisha na kuongeza bao jingine. Mchezo wa hatua ya 16 bora kati ya Senegal na Sudan ulimalizika kwa Senegal kushinda kwa mabao 3–1. Mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Grand Stade de Tanger ulikuwa na ushindani mkubwa ambapo Senegal walipata jumla ya kona 7, huku Sudan wakipata kona 4 ndani ya dakika 90. Cameroon pia imetinga hata ya robo fainali baada ya kuichakaza Afrika Kusini mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa Jumapili katika Uwanja wa Agdal Medina jijini Rabat. Mabao wa Indomitable Lions yalifungwa na Junior Tchamadeu katika dakika ya 34 na Christian Kofane kunako dakika ya 47. Bao la kufitia machozi la Bafana Bafana lilifungwa na Evidence Makgopa katika dakika za lala salama kipindi cha pili. Cameroon sasa itachuana na mwenyeji Morocco katika robofainali ya kwanza Ijumaa, huku robofainali nyingine ikizichuanisha Mali na Senegal siku hiyo hiyo.  Jumanne hii, DRC itatoana udhia na Algeria kusaka tiketi ya robo fainali, wakati ambapo Ivory Coast itakuwa inacheza na Burkina Faso. Nusu fainali zitapigwa Jumatano ya juma lijalo, huku mchezo wa kutafuta mshindi wa 3 wa michuano ya AFCON 2025 ukisakatwa Jumamosi. Simba wa Afrika kwenye mpira wa miguu atajulikana Jumamosi ya Januari 18.

Wanamichezo wa Uturuki waitetea Palestina

Wanachama wa jamii ya michezo ya Uturuki walijiunga na mkutano mkubwa siku ya Alhamisi kwenye Daraja la Galata la Istanbul kuelezea mshikamano na Palestina, wakitaka kukomeshwa kwa ghasia zinazoendelea katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Maandamano hayo yaliandaliwa na Muungano wa Ubinadamu na Jukwaa la Utashi wa Kitaifa chini ya kauli mbiu: "Hatutaogopa, hatutanyamaza, hatutasahau Palestina." Tukio hilo likiongozwa na Wakfu wa Vijana wa Türkiye (TUGVA) lilileta ushiriki mkubwa kutoka kwa wanariadha, maafisa wa michezo na wawakilishi wa klabu. Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na Waziri wa Vijana na Michezo Osman Askin Bak, Rais wa Shirikisho la Mieleka la Uturuki Taha Akgul, Rais wa Shirikisho la Karate la Uturuki Ercument Tasdemir, Rais wa Besiktas Serdal Adali, Wajumbe wa bodi ya Fenerbahce Ertan Torunogullari, Adem Koz, Ilker Alkun, na Taner Sonmezer, Naibu Mwenyekiti wa Galatasaray Gavulah Kavuray, Kocha Mkuu wa Galatasaray, Gavuray Gavukata AS. Buruk, mwanamieleka wa kitaifa Riza Kayaalp, pamoja na watendaji na wanariadha wengi kutoka mashirikisho ya michezo na vilabu.

 

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Bak alisema Türkiye amekuwa akisimama karibu na watu wanaokandamizwa, akibainisha kuwa Rais Recep Tayyip Erdogan amezungumzia hali ya Gaza katika Umoja wa Mataifa na majukwaa mengine ya kimataifa. "Usikivu unaoonyeshwa na watu wetu kuelekea Gaza ni muhimu sana," Bak alisema. "Wananchi kutoka kote nchini wanakusanyika hapa ili kutoa sauti zao." Akisisitiza jukumu la kuunganisha la michezo, Bak alishukuru vilabu na wanariadha kwa ushiriki wao. "Vijana wetu kuchukua umiliki wa jambo hili ni muhimu sana," alisema. Kocha mkuu wa Galatasaray Buruk alisema watu wa Uturuki daima wamesimama na Palestina. "Tunashiriki maumivu yao," Buruk alisema. "Ina maana kuona wafuasi wa timu tofauti wamekusanyika hapa kuonyesha mshikamano."

 

Dondoo za Hapa na Pale

Mchezaji nyota wa tenisi kutoka Kenya, Angella Akutoyi ameibuka kidedea katika mashindano ya dunia ya World Tour Nairobi (W35) yaliyoandaliwa na Shirikisho la Tenisi Duniani ITF. Okutoyi mwenye umri wa miaka 21 alibubujikwa na machozi baada ya kumbwaga Martina Colmegna wa Italia anayeshika nafasi ya nne duniani, kwa kumchabanga seti za 6-3, 3-6, 6-3. Huo ulikuwa ushindi wa kwanza wa Okutoyi katika W35 baada ya majaribio sita mwaka jana huko Nairobi, Uholanzi, na Marekani.

 

Kwengineko, klabu ya soka ya Uingereza Chelsea ilisema Alkhamisi kwamba imemtema kocha mkuu Enzo Maresca, ikimtakia Muitaliano huyo kila heri katika maisha yake ya baadaye. Katika taarifa yake, Chelsea ilisema Maresca, 45, alifurahia mafanikio makubwa katika kipindi chake cha uongozi, na kuiongoza timu hiyo kupata ushindi katika Ligi ya Mabingwa ya UEFA na Kombe la Dunia la Vilabu la FIFA.

Enzo Maresca aliyetimuliwa Chelsea

 

"Mafanikio hayo yatabaki kuwa sehemu muhimu ya historia ya hivi karibuni ya klabu hii, na tunamshukuru kwa michango yake," ilisema taarifa hiyo. Klabu hiyo iliongeza kuwa, ikiwa na malengo muhimu bado ya kucheza kwa mashindano yote manne, pamoja na kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa ya UEFA msimu ujao, pande zote mbili zilikubaliana kwamba mabadiliko ya usimamizi yataipa timu nafasi nzuri ya kurejea kwenye mkondo.

Na Msemaji wa Shirikisho la Soka la Iran, Amirmehdi Alavi, amethibitisha ratiba ya mechi ya kirafiki kati ya Iran na Uhispania mnamo Juni 2 katika Uwanja wa Metropolitano mjini Madrid, Uhispania. Mechi hii ni sehemu muhimu ya maandalizi ya kikosi cha Iran kinachofahamika hapa nchini Timu Melli kwa Kombe la Dunia la FIFA la 2026, ambapo wamepangwa katika Kundi G pamoja na Ubelgiji, Misri na New Zealand.

Timu zitakazoshiriki Kombe la Dunia 2026

 

Iran itajaribu kupima ujuzi wake dhidi ya moja ya vigogo wa soka barani Ulaya, katika juhudi za kurekebisha mbinu zao na kuisuka timu kabla ya mashindano ya kimataifa ya FIFA. Msemaji wa Shirikisho la Soka la Iran amesema mechi hiyo ya kirafiki litakuwa pambano la kusisimua, likitoa uzoefu muhimu kwa pande zote mbili wanapojiandaa kwa michuano mikali iliyopo mbele yao.

………………………TAMATI……………..