Ulimwengu wa Spoti, Feb 9
https://parstoday.ir/sw/news/event-i136432-ulimwengu_wa_spoti_feb_9
Natumai hujambo msikilizaji mpenzi na karibu tutupie jicho matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa.
(last modified 2026-02-09T11:19:05+00:00 )
Feb 09, 2026 07:08 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Feb 9

Natumai hujambo msikilizaji mpenzi na karibu tutupie jicho matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa.

Futsal fainali: Iran vs Indonesia

Timu ya taifa ya wanaume ya Iran ya futsal imetwaa ubingwa wa mchezo huo barani Asia kwa mara nyingine tena. Hii ni baada ya kuishinda timu mwenyeji Indonesia kwa mikwaju ya penalti katika fainali nzito iliyopigwa siku ya Jumamosi. Iran, ambao ni mabingwa watetezi, walikabiliana kufa kupona na wenyeji, katika fainali hiyo ya Kombe la Asia la AFC Futsal 2026, na kutoka sare ya mabao 5-5 katika muda wa kawaida na muda wa nyongeza. Hatimaye, Iran iliwashinda Waindonesia kupitia mikwaju ya penalti kwa kuwazaba mabao 6-5.

Iran mabingwa wa Futsal Asia 2026

 

Iran ilitinga fainali baada ya kushinda Iraq kwa mabao 4-2 katika nusu fainali yao siku ya Alhamisi. Siku hiyo hiyo, Indonesia iliitandika Japan mabao 5-3 katika nusu fainali ya pili ya mashindano hayo ya kibara ya Kombe la Asia la AFC Futsal Indonesia 2026. Viongozi mbali mbali wa Iran, wakiwemo Rais Masoud Pezeshkian, Spika wa Bunge la Iran, Muhammad Baqer Qalibaf na Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi wameipongeza timu hiyo ya Iran kwa kuibuka kidedea katika mashindano hayo na kuipepersusha bendera ya Jamhuri ya Kiislamu kwa mara nyingine tena.

Mieleka: Iran yachota medali lukuki

Mwanamieleka nyota wa Iran, Erfan Jarkani alishinda medali ya dhahabu Ijumaa katika kategoria ya kilo 63 katika Mashindano ya Mieleka ya Wazi ya Greco-Roman yaliyoandaliwa na Shirikisho la Mieleka Duniani (UWW) huko Zagreb, Croatia. Jarkani alionyesha umahiri wake kwenye mapambano yake, akiwashinda Saifullah Kurman wa Kazakhstan (10-1), Khusniddin Olimbov wa Uzbekistan (9-1), na Vitalie Eremenko wa Moldova (3-1) na kufikia fainali. Alimchakaza Chetan Chetan wa India kwa alama 8-4 katika ngoma ya fainali na kushinda dhahabu.

 

Katika uzito huo huo, Meysam Delkhani wa Iran alipata medali ya shaba baada ya kumshinda Dastan Zarlykhanov wa Kazakhstan kwa 8-0 katika mgaragazano wa kumtafuta mshindi wa shaba. Aidha bingwa wa mieleka mtindo wa Greco-Roman wa Iran, Ali Oskou, alishinda medali ya dhahabu katika mashindano hayo ya Zagreb Open Jumamosi usiku, baada ya kumpeleka mchakamchaka mwanamieleka wa Hungary, Zoltan Levai na kumshinda kwa alama 9-1 katika pambano la fainali la kilo 77. Wakati huo huo, mwanamieleka wa Iran Hassan Yazdani alishinda medali ya fedha katika mashindano hayo ya Zagreb Open 2026 siku ya Alhamisi. Michuano ya Zagreb Open ya 2026 iliyopigwa katika Uwanja wa Arena Zagreb nchini Croatia , ilianza Februari 4 na kufunga pazia lake Februari 8.

Soka Afrika; Simba na Naibois walala

Klabu ya soka ya Simba Sc ya Tanzania imebanduliwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya Shirikisho la Soka barani humo CAF, kufuatia sare ya bao 1-1 dhidi ya Petro De Luanda ya Angola kwenye mchezo wa kundi D uliopigwa wikendi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Masaibu ya mashabiki wa Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika yalikolea mwishoni mwa mwezi uliopita wa Januari, baada ya timu hiyo kufungwa bao 1-0 na Espérance de Tunis ya Tunisia kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika nchini Tunisi.

Wekundu wa Msimbazi wamefikisha alama mbili tu baada ya mechi tano kwenye kundi hilo huku wakisalia na mchezo mmoja wa kukamilisha ratiba. Baadhi ya wachambuzi wanahisi kwamba Simba walijitihadi kwenye mchezo huo wa wikendi, kwani walicheza pungufu kwa karibu dakika 50 baada ya beki Shomari Kapombe kulishwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza.  

 

Kufuatia matokeo hayo, ndoto za Simba SC za kusonga mbele katika michuano hiyo zimefikia tamati baada ya kushindwa kufikisha idadi ya pointi zinazohitajika. Stade Malien ya Mali inaongoza Kundi D baada ya kucheza mechi 4, huku wakiwa na pointi 8, wakifuatiwa na Esperance wenye alama 6 baada ya kucheza mechi 4. Nafasi ya tatu kwenye kundi hilo inashikiliwa na Petro Luanda ambao pia wana alama 6 baada ya kucheza mechi 5, huku Simba wakivuta mkia kundini kwa alama 2 baada ya kusakata michuano 5, na ni timu pekee ambayo haijashinda mchezo wowote kwenye kundi lao. Wanasimba walikuwa na haya ya kusema baada ya sare hiyo na Waangola.

Wakati huo huo, mchezo wa AS FAR Rabat na Yanga ya Tanzania uliopigwa katika Uwanja wa Mwanamfalme Moulay Abdillah nchini Morocco ulimalizika kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Kutokana na matokeo hayo Wamorocco wamefikisha pointi nane na kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi B na kuiacha Yanga ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi tano. Kundi hilo linaongozwa na Al Ahly yenye pointi tisa. Nafasi ya Yanga kufuzu robo fainali inatagemea matokeo ya mchezo wake wa mwisho dhidi ya JS Kabylie utakaopigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ikitakiwa ishinde huku ikiiombea AS FAR Rabat ipoteze kwa Al Ahly, na kisha Yanga ishindane na AS FAR Rabat uwiano wa magoli ya kufunga na kufungwa, maana wote watakuwa na pointi nane, muhali kabisa? Baada ya watani hao wa jadi kutimuliwa mavumbi kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, klabu ya Azam FC ya Dar es Salaam, imeitoa kimasomaso Tanzania kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS Maniema kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika uliotandazwa katika Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar. Kwa ushindi huo, Azam imefikisha pointi tisa kundini.

Wakati huo huo, klabu ya Nairobi United ya Kenya, ambayo hana pointi katika Kundi B, alikabiliana na miamba wa soka kutoka Morocco, klabu ya Wydad Casablanca katika Uwanja wa Nyayo Jumapili na kulimwa bao bao moja kwa nunge. 'Naibois' kama wanavyofahamika hapo Kanairo, wanatazamiwa kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Februari 15 kucheza na AS Maniema Union katika mchuano wa kamilisha ratiba.

Kwa ushindi huo wa Jumapili, Wydad wanaongoza Kundi B kwa alama 12, wakifuatiwa na Maniema Union wenye alama 9, pointi sawia na Azam ya Tanzania ambayo inafunga orodha ya tatu bora.

Katika hatua nyingine, timu ya soka ya majanajike ya Rising Starlets ya Kenya haitakuwa na presha sana katika mchezo wa pili wa kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake la FIFA, kwa wachezaji wenye chini ya umri wa miaka 20, baada ya Elizabeth Mideva kuifungia timu hiyo bao la kipekee katika dakika za lala salama, na kuwapa wenyeji ushindi mgumu wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania katika Uwanja wa Ulinzi Sports Complex Jumamosi. Baada ya Tanzania kuwachezesha washambuliaji hatari katika kipindi cha pili, huku wageni wakiongeza mashinikizo uwanjani wakitafuta bao la ugenini, lakini safu ya ulinzi ya Kenya ilibaki imara. Matokeo hayo yanaifanya timu hiyo kuwa katika hali nzuri kabla ya mechi ya marudiano iliyopangwa kufanyika Februari 14 katika Uwanja wa Azam Complex jijini Dar-es-salaam.

Dondoo za Hapa na Pale

Meneja wa timu ya Manchester City, Pep Guardiola alisisitiza Ijumaa hii kwamba atapaza sauti yake waziwazi wakati wowote "watu wasio na hatia wanapouawa" popote pale duniani, akijibu ukosoaji wa Baraza la Wawakilishi wa Jumuiya ya Wayahudi la Jiji la Manchester nchini Uingereza. "Kwa nini siruhusiwi kuelezea hisia zangu? Kwa sababu tu mimi ni kocha? Sikubaliani na jambo hilo, lakini naheshimu maoni yote," amesema Guardiola na kuongeza kwamba: "Watu wasio na hatia wanauawa, na ninalaani vikali jambo hilo." Tamko hilo la Guardiola linakuja kujibu ukosoaji wa Bodi ya Wawakilishi wa Kiyahudi ya Greater Manchester kufuatia matamshi aliyotoa kabla ya mchezo wa pili wa nusu fainali ya Kombe la Carabao kati ya Manchester City na Newcastle Jumatano iliyopita.

Meneja wa timu ya Manchester City, Pep Guardiola, mtetezi wa Palestina

 

Na nikudokeza, klabu ya soka ya Arsenal itavaana na Manchester City hiyo katika fainali ya Kombe la Carabao. Fainali hiyo ya ndovu kumla mwanawe itachezwa huko Wembley mwezi ujao. Wabeba Bunduki walitinga fainali ya Kombe la Carabao baada ya kuizabana Chelsea bao 1 bila jibu siku ya Jumatano. Bao la Kai Havertz la dakika ya 96 liliwapa Gunners ushindi wa 1-0 dhidi ya Blues katika mchezo uliowahakikishia Wabeba Bunduki nafasi yao katika fainali itakayochezwa Wembley.

Manchester City iliishinda Newcastle United mabao 3-1 katika Uwanja wa Etihad na kushinda jumla ya mabao 5-1 katika mchezo wao pili wa nusu fainali ya Kombe la Carabao. Mabao mawili ya mapema ya Omar Marmoush na la Tijjani Reijnders yaliisaidia City kujikatia tiketi ya kushuka Wembley dhidi ya Arsenal katika fainali itakayopigwa mnamo Machi 22. Newcastle ilipata bao la kufutia machozi kunako dakika ya 62 kupitia Anthony Elanga. Mambo yanazidi kuwaendelea vizuri Gunners hata kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Viktor Gyokeres alifunga mabao mawili huku Arsenal ikiishinda Sunderland bila tabu na panua mwanya wa uongozi wao kileleni mwa jedwali la EPL kwa pointi 6. Mwanya huo hata hivyo Jumapili uliipunguzwa tena na Man City iliyowashukiwa vibaya Liverpool licha ya kuupigia nyumbani Anfield. Mabao ya City yalifungwa na Bernado Silva na mkwaju wa penati wa Earling Halaand katika dakika za lala salama, ingawaje wenyeji walikuwa wa kwanza kucheka na nyavu kupitia goli la Dominiki Szoboloszlai katika dakika ya 74 ya mchezo.

Wakati huohuo, Manchester United imeendeleza rekodi ya ushindi chini ya mkufunzi mpya Michael Carrick. Bryan Mbeumo aliiweka United kifua mbele kunako baada ya dakika 38 ya mchezo walipovaana na Spurs huko Old Trafford, huko Bruno Farnandes akiwaongeza Mashetani Wekundu la pili. Kocha Ruben Amorim hajawahi kushinda michezo minne mfululizo akiwa meneja wa United.

Baadhi ya wanamichezo wa Iran katika Michezo ya Olimpiki

 

Mbali na hayo, timu ya wanariadha na wanamichezo wengine wa Utawala wa Kizayuni wa Israel ulizomewa ilipoingia uwanjani wakati wa sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Msimu wa Baridi Kali huko MIland nchini Italia. Maelfu ya mashabiki waliofurika uwanjani waliizomea timu hiyo ya Israel, kutokana na jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Hali kadhalika, Makamu wa Rais Marekani, JD Vance alizomewa pia uwanjani hapo, kutokana na kile wadadisi wa mambo wanasema ni kuendelea kuporomoka hadhi na ushawishi wa Marekani katika uga wa kimataifa.

Na mashabiki kumi na wanane wa mpira wa miguu wa Senegal waliokamatwa nchini Morocco kwa "uhuni" wakati wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwezi uliopita wameanza mgomo wa kula wakisubiri kesi yao. Wakili Patrick Kabou amesema wateja wake walimwambia wamekuwa "wakisubiri kujua mashtaka dhidi yao tangu Januari 18", siku waliyokamatwa baada ya fainali kali ya AFCON ambapo Senegal iliifunga Morocco mjini Rabat.

…………………TAMATI………….….