Ulimwengu wa Spoti, Feb 16
https://parstoday.ir/sw/news/event-i136696-ulimwengu_wa_spoti_feb_16
Hujambo mpenzi mwanaspoti na karibu tuzamie baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyoshuhudiwa ndani ya siku saba zilizopita katika pembe tofauti za dunia.
(last modified 2026-02-16T10:57:41+00:00 )
Feb 16, 2026 10:56 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Feb 16

Hujambo mpenzi mwanaspoti na karibu tuzamie baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyoshuhudiwa ndani ya siku saba zilizopita katika pembe tofauti za dunia.

Muaythai: Iran yavuna dhahabu lukuki

Timu ya Muaythai ya Iran imekamilisha kampeni yake katika Michezo ya Wazi ya Masters Abu Dhabi 2026, ikimaliza na ushindi wa kuvutia kwa kuvuna medali tisa za dhahabu na tatu za fedha. Ikiwa na wanamichezo 11 wa kiume na wa kike, timu ya Iran ilionyesha umahiri wake katika kategoria nyingi za uzito, wakati wa mashindano hayo yaliyoanza Februari 6 na kufunga pazia lake Febnruari 15 kati ka Umoja wa Falme za Kiarabu.

Timu ya muaythai ya Iran

 

Medali za dhahabu za Jamhuri ya Kiisilamu zilitwaliwa na Hadi Mohammadzadeh (kilo –91), Ali Mousavi (kilo –75), Mehdi Qolizadeh (kilo –81), Hossein Karami (kilo –81), Saeed Afrasiabi (kilo –86), Shahram Dalvand (kilo –91), na Yousef Soltani (kilo +91). Medali za fedha za Iran zilitwaliwa na Ghadir Mirshamsi, Peyman Papi, na Ferdows Shokouhi.

Ligi ya Soka ya Wanawake

Klabu ya mpira wa miguu ya Bam Khatoon imeshinda duru ya 18 ya Ligi Kuu ya Soka la Wanawake ya Iran. Timu hiyo yenye makao yake makuu huko Bam, ilishinda taji hilo ikiwa na pointi 52 katika ligi hiyo ya timu 10.

Klabu ya kandanda ya Bam Khatoon ya Iran

 

Khatoon iliishinda Sepahan na kushinda taji hilo kwa mabao 2-1. Hili lilikuwa taji la 11 la timu hiyo ya soka ya wanawake ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Futsal: Yakwea hadi nafasi ya 4

Timu ya taifa ya futsal ya Iran imekwea hadi katika nafasi ya nne kwenye orodha ya hivi punde ya viwango ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA kwa jumla ya pointi 1,523. Orodha hiyo ya viwango vya kimataifa iliyosasishwa ya futsal ilitolewa kufuatia kumalizika kwa Ligi ya Euro, Copa América, na mashindano ya Kombe la Asia la Shirikisho la Kandanda Asia AFC.

Timu ya futsal ya Iran ikishangilia bao

 

Brazil, Uhispania, Ureno, Iran, Argentina, Morocco, Russia, Kazakhstan, Ukraine, na Ufaransa zinashika nafasi kumi za kwanza mtawalia kwenye orodha hiyo. Iran, ambayo hapo awali iliorodheshwa ya tano, ilipanda nafasi moja baada ya kushinda ubingwa wa Asia mwaka huu 2026. Iran pia imedumisha nafasi yake kama timu bora zaidi ya futsal ya Asia, huku Thailand, Japan, na Indonesia zikishika nafasi ya pili hadi ya nne kwa usanjari huo barani hapa.

Mabingwa Afrika; Simba nje licha ya ushindi

Licha ya klabu ya Simba SC ya Tanzania kupata ushindi wa kwanza kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya Shirikisho la Kandanda Afrika (CAF), lakini hilo halikuwafanya Wekundu wa Msimbazi wapone kisu cha kubanduliwa nje ya michuano hiyo. Simba ilivuna ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya vinara wa kundi D, Stade Malien ya Mali katika Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam wikendi. Simba ilipata bao hilo mapema, kupitia Anicet Oura. Ushindi huo unakuja wiki moja baada ya Simba kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Petro De Luanda ya Angola kwenye mchezo wa kundi D uliopigwa pia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwenye mchezo mwingine wa kundi hilo, Esperance de Tunis ya Tunisia imeilaza Petro De Luanda ya Angola mabao 2-0 na kuungana na Stade de Malien ya Mali kwenye hatua ya robo fainali; huku Simba na Petro Luanda kuaga mashindano hayo.

Hali kadhalika, Young Africans Sc wamebanduliwa kwenye ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) baada ya Al Ahly kutoshana nguvu na AS Far Rabat kwa sare tasa. Hii ni licha ya Yanga Sc kushinda kwa kishindo dhidi ya JS Kabylie katika mechi iliyopigwa katika dimba la New Amaan Complex, Zanzibar.

 

AS Far Rabat ya Morocco wameungana na Al Ahly ya Misri kwenye robo fainali ya michuano hiyo huku Yanga Sc ikiungana na Simba Sc, Azam FC na Singida Black Stars kurudi nyumbani baada ya timu zote kutoka Tanzania kuaga michuano ya CAF. Azam FC ya Tanzania ilisukumizwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCL) kufuatia kipigo cha mabao 2-0 ugenini dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco kwenye mchezo wa mwisho wa kundi B.

Kwenye mchezo mwingine wa kundi hilo, Nairobi United ya Kenya imekamilisha ratiba kwa kipigo cha mbgwa kuingia msikitini, cha magoli 3-0 dhidi ya Maniema ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wakati huo huo, klabu ya Al Ahly ya Misri siku ya Jumapili ilitoana jasho na AS FAR Rabat ya Morocco katika mchezo wa Ligi ya Klabu Bingwa Afrika. Kwenye mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Kimataifa Cairo, na kutajwa kuwa miongoni mwa mechi zilizovuta hisia kubwa barani Afrika, ulimalizika kwa vigogo hao kutoa sare tasa.

Ndoto ya Starlet Kombe la Dunia yazimwa

Ndoto ya timu ya soka ya majanajike ya Rising Starlets ya Kenya ya kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake la FIFA 2026, kwa wachezaji wenye chini ya umri wa miaka 20 imezimwa. Hii ni baada ya kuzabwa na Tanzania Queens kwenye upigaji matatu katika mechi ya marudiano iliyopigwa wikendi katika Uwanja wa Azam Complex jijini Dar-es-salaam. Rising Starlets walikuwa na faida ya bao moja katika mechi hiyo ya mkondo wa pili baada ya kuizaba Tanzania bao moja bla jibu katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa katika Uwanja wa Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi Jumamosi ya wiki iliyopita. Timu hizo zilizotoa sare ya bao 1-1 katika dakika za ada na nyongeza kabla ya kuigia kwenye upigaji penati. Mabanati hao wa Tanzania wamefuzu kwa raundi nne na ya mwisho ya kuwania tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia, baada ya kuicharaza Kenya jumla ya magoli 3-1, na sasa watanazamiwa kuvaana na Cameroon mwezi Mei. Cameroon walitinga raundi ya mwisho baada ya kuichachafya Botswana jumla ya mabao 5-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza na wa pili.

AFCON kuakhirishwa?

Kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), imethibitisha kuwa michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika 2027 haitaahirishwa, licha ya kuwepo kwa wasiwasi kuhusiana na maandalizi ya Miundombinu na hali ya hewa ya kisiasa katika nchi waandaaji. Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika Juni-Julai mwakani, licha ya wito kutoka kwa Mwenyeji mwenza Kenya kufikiria kuahirishwa kutokana na hatari ya vurugu zinazohusishwa na Uchaguzi uliopangwa kufanyika kwa muda huo.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe

 

CAF imesalia kuwa na msimamo imara, huku timu ya ukaguzi ikiendelea na kazi yake katika nchi tatu za Tanzania,Kenya na Uganda. CAF imesisitiza dhamira yake ya kuimarisha Waamuzi na Nidhamu, maeneo mawili yaliyochukuliwa kuwa muhimu ili kuhakikisha uaminifu wa mashindano ya Afrika. Kulikuwa na wasi wasi juu ya kuwepo uwezekano mkubwa wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 nchini Kenya, Uganda na Tanzania ikaakhirishwa. Kazi kubwa za ujenzi kwa sasa zinaendelea katika viwanja vipya kama Talanta (Nairobi) na Samia Suluhu (Arusha).

 Dondoo za Hapa na Pale

Klabu ya Atletico Madrid iliilaza Barcelona mabao manne katika kipindi cha kwanza na kupata ushindi wa 4-0 katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Copa del Rey, na kuwaacha haoi mabingwa hao watetezi vinywa wazi katika mechi ya marudiano. Kikosi cha Diego Simeone kilihitaji dakika 45 pekee nyumbani ili kudhibiti mechi hiyo Alkhamisi, wakitumia vibaya kosa la mapema, kabla ya kuiongoza timu ya Hansi Flick kufungua mlango kwa hiari yao ili kuelekea ukingoni mwa fainali ya Aprili huko Seville.

 

Atletico sasa watakutana na Real Sociedad au Athletic Bilbao katika ngoma nzito ya fainali. Real Sociedad wana faida ya 1-0 kabla ya mechi yao ya marudiano huko San Sebastian mnamo Machi 4.

Katika riadha, mwanariadha nyota wa Kenya, Faith Kipyegon ameshinda mbio zake za kwanza za kilomita 10 za barabarani huko Monaco.  Afande Kipyegon mwenye miaka 32, aliibuka kidedea kwenye mashindano hayo Jumapili huko Monacho nchini Ufaransa, kwa kutumia dakika 29, na sekunde 47, akimtifulia mavumbi Mtaliano Mattia Gugliemi aliyemaliza wa pili kwa kutumia dakika 32 na sekunde 32.32.

Kwengineko, Shirikisho la Soka la Iran linatarajiwa kutangaza rasmi ratiba ya mechi za kirafiki za timu ya kandanda ya Jamhuri ya Kiislamu huku maandalizi ya Kombe la Dunia la FIFA la 2026 yakishika kasi. Inaarifiwa kuwa, shirikisho hilo linafanya mazungumzo na mashirikisho ya soka ya Costa Rica na Nigeria ili kupanga mechi mbili za kupasha moto misuli mwezi Machi, gazeti la Tehran Times limeripoti. Awali ilipendekezwa kuwa Iran itakabiliana na vigogo wa Ulaya Uhispania na Ureno katika mechi za maandalizi. Pia kulikuwa na majadiliano ya Iran kuchuana na Senegal katika mechi ya kirafiki, ingawa hakuna makubaliano ya mwisho yaliyothibitishwa. Iran imepangwa Kundi G, pamoja na miamba ya soka duniani Ubelgiji, Misri, na New Zealand.

Na timu ya kriketi ya Zimbabwe iliisagasaga Australia kwa mikimbio 23 mjini Colombo na na kuvuna ushindi wa kishindo na ulioshangaza dunia mpaka sasa katika Kombe la Dunia la T20. Baada ya kufikisha pointi 169-2 katika over zao 20 siku ya Ijumaa, hasa kutokana na Brian Bennett kutotoka nje kwa pointi 64, Zimbabwe iliifanya Australia kuwa na pointi 29-4 kabla ya kuwatimulia mavumbi kwa pointi 146 katika over 19.3.

 

Zimbabwe, walio katika nafasi ya 11, walikuwa na udhibiti kila mara dhidi ya wapinzani wao walio katika nafasi ya pili katika mchezo wa Kundi B katika Uwanja wa R Premadasa baada ya wachezaji Blessing Muzarabani na Brad Evans kuwashinda wapinzani wao wakubwa wa Australia. Zimbabwe iliichakaza Oman katika mchezo wao wa ufunguzi.

……………….TAMATI…………..