Uchaguzi wa rais Cameroon kufanyika mwezi Oktoba
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128228-uchaguzi_wa_rais_cameroon_kufanyika_mwezi_oktoba
Serikali ya Cameroon imetangaza kuwa uchaguzi wa urais utafanyika tarehe 12 Oktoba. Hayo ni kwa mujibu wa amri iliyosainiwa Ijumaa na Rais Paul Biya.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Jul 12, 2025 04:08 UTC
  • Uchaguzi wa rais Cameroon kufanyika mwezi Oktoba

Serikali ya Cameroon imetangaza kuwa uchaguzi wa urais utafanyika tarehe 12 Oktoba. Hayo ni kwa mujibu wa amri iliyosainiwa Ijumaa na Rais Paul Biya.

Biya, mwenye umri wa miaka 92, ndiye kiongozi mkuu wa nchi aliye madarakani kwa muda mrefu zaidi duniani, na amekuwa mamlakani kwa zaidi ya miaka 40 tangu alipoingia madarakani mwaka 1982. Hadi sasa, hajatangaza kama atawania tena urais, ingawa mageuzi ya kikatiba ya mwaka 2008 yaliondoa kikomo cha mihula ya urais.

Mwaka 2018, alishinda uchaguzi kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura, ingawa uchaguzi huo ulikumbwa na dosari nyingi na kiwango cha chini cha ushiriki kutokana na mashambulizi ya waasi wa makundi yanayotaka kujitenga na makundi ya kigaidi.

Biya mara kwa mara husafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, na mwaka jana uvumi ulienea kwamba alikuwa amefariki dunia, uvumi ambao serikali iliukanusha vikali hadharani.

Kwa kuwa tarehe ya uchaguzi sasa imewekwa rasmi, vyama vya siasa tayari vimeanza kujipanga. Wagombea kadhaa wameshatangaza nia ya kuwania urais, akiwemo Waziri wa zamani wa Mawasiliano, Issa Tchiroma Bakary, ambaye alijiuzulu mwezi uliopita.

Waziri wa Utalii , Bello Bouba Maigari, naye amekubali uteuzi wa chama chake kuwania urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

Mpinzani mkuu wa Biya anatarajiwa kuwa Maurice Kamto, ambaye ameendelea kufanya kampeni nchi nzima licha ya vitisho vya mara kwa mara kutoka kwa polisi. Tukio la hivi karibuni lilitokea aliporejea kutoka Ulaya alikokuwa akifanya kampeni, ambapo mamia ya askari polisi walimzuia kutoka makao makuu ya chama chake ili kuzuia mikutano aliyopanga kufanya katika jiji la Douala.

Uchaguzi ujao unaweza kuwa hatua ya mabadiliko makubwa kwa nchi ambayo, tangu kupata uhuru wake, imewahi kuwa na marais wawili tu—mmoja kutoka kusini mwa nchi ambako Wakristo wengi wanaishi, na mwingine kutoka kaskazini yenye idadi kubwa ya Waislamu. Rais wa kwanza wa Cameroon alikuwa Ahmadou Babatoura Ahidjo kutoka eneo la kaskazini.