Polisi ya Uturuki yazima njama ya mauaji dhidi ya Rais Erdogan
Vyombo vya habari vya Uturuki vimeripoti kuwa, polisi ya nchi hiyo imegundua na kulipua bomu lililokuwa limetegwa eneo ambako Rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdoğan, alipangiwa kuhutubia wananchi huko kusini mwa Uturuki.
Polisi ya Uturuki imesema kuwa bomu hilo lilitengwa ndani ya gari linalomilikiwa na polisi na kwamba uchunguzi mkubwa unafanyika kubaini undani wa tukio hilo.
Kwa sasa Uturuki inasumbuliwa na hali ya mivutano kutokana na migogoro ya kiuchumi inayosababishwa na kuporomoka kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo.
Lira ya Uturuki imepoteza asilimia 44 ya thamani yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa karibuni mkabala wa dola ya Marekani na Rais Erdogan amewatimua kazi wakuu wa tatu wa Benki Kuu ya nchi hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Siku chache zilizopita pia Rais wa Uturuki alimpiga kalamu nyekundu Waziri wa Uchumi wa nchi hiyo.