Russia yalipiza kisasi, yawafukuza wanadiplomasia 45 wa Poland
Wizara ya Mambo ya Nje wa Russia imetangaza kuwa imewafukuza wanadiplomasia 45 wa Polanda waliokuweko nchini humo ikiwa ni majibu ya hatua kama hiyo iliyochukuliwa na nchi za Magharibi dhidi yake.
Shirika la habari la FARS limeripoti habari hiyo na kunukuu taarifa ya jana Ijumaa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ikisema kuwa, Moscow imeamua kuwatimua wanadiplomasia 45 wa Poland waliokuweko kwenye ubalozi na balozi ndogo za Poland nchini humo ikiwa ni kulipiza kisasi kwa hatua kama hiyo iliyochukuliwa na Poland dhidi ya wanadiplomasia wa Russia.
Vile vile wizara hiyo ya mambo ya nje ya Russia imesema, imewatimua wanadiplomasia wawili wa Bulgaria waliokuweko mjini Mascow ikiwa pia ni kulipiza kisasi kwa hatua kama hiyo iliyochukuliwa na Bulgaria dhidi ya wanadiplomasia wa Russia.
Vita vya kidiplomasia vinaendelea baina ya nchi za Magharibi na Moscow tangu Russia ilipoanzisha operesheeni ya kijeshi nchini Ukraine. Baadhi ya nchi za Ulaya zimeamua kuwafukuza wanadiplomasia wa Russia katika nchi hzo, hatua ambayo tab'an isingeliachwa vivi hivi bila ya kujibiwa na Moscow.
Kabla ya hapo pia shirika la habari la Tass lilikuwa limeripoti kuwa, Bunge la Ulaya limepiga marufuku kuingia katika makao makuu ya bunge hilo wanadiplomasia na viongozi kutoka Russia na Belarus.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema pia kuwa, ni haki ya Moscow kuchukua hatua yoyote ya kulipiza kisasi kwa kila nchi ya Ulaya inayofukuza wanadiplomasia wake.
Mara chungu nzima nchi za Ulaya kwa kuifuata kibubusa Marekani zimekuwa zikichukua hatua kama hiyo dhidi ya wanadiplomasia wa Russia kwa visingizio tofauti.