Russia: Suala la nyuklia linaweza kutatuliwa kwa kuzingatia maslahi ya Iran
-
Maria Zakharova
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova, anasema kwamba mgogoro unaoendelezwa na Marekani kuhusu suala la nyuklia la Iran unaweza tu kutatuliwa kwa njia za kidiplomasia na kwa kutilia maanani maslahi ya Iran.
Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari mjini Zakharova alisema kuwa "suala la nyuklia la Iran linaweza tu kutatuliwa kwa njia za kisiasa na kidiplomasia, kwa kuzingatia sheria za kimataifa na kwa kuzingatia maslahi ya Iran."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesisitiza "msimamo mkuu wa Russia kuhusu haki halali na isiyopingika ya Iran ya kuendeleza shughuli za nyuklia kwa malengo ya amani kwa mujibu wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT)."
Zakharova amesisitiza kuwa ni Iran pekee inayopasa kuamua hatima ya akiba yake ya urani katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati yake na Marekani.
“Ni wananchi wa Iran wenyewe ambao wanaweza kutoa maamuzi kuhusu haki yao hiyo likiwemo suala la urutubishaji urani,” ameongeza Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia.
Bi Zakharova amesema kuwa Moscow imejiandaa kusaidia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani na kwamba Russia iko tayari kikamilifu kuzisaidia Tehran na Washington kuchukua maamuzi kuhusu urani iliyorutubishwa.