Russia yawapatia wanajeshi wa Ukraine makataa mapya ili kujisalimisha huko Mariupol
Russia imewapatia makaa mapya wanajeshi wa Ukraine ambao bado wapo katika mji wa kistratejia wa bandari wa Mariupol huko Kusini mwa Ukraine; huku Moscow ikiendeleza mashambulizi yake upande wa Mashariki mwa nchi hiyo.
Vikosi vya ulinzi vya Russia ambavyo kimsingi vinazingatia kanuni za kibinadamu, kwa mara nyingine tena vimependekeza kuwa, wapiganaji wazalendo wa Ukraine na mamluki wa nchi za kigeni wanapasa kusitisha mashambulizi yao na kuweka chini silaha kuanzia sasa 8 mchana siku ya Jumatano wiki hii kwa wakati wa Moscow. Hayo yameelezwa na Wizara ya Ulinzi ya Russia.
Wizara ya Ulinzi ya Russia imetoa makataa hayo mapya kwa Ukraine baada ya yale ya awali kumalizika muda wake. Imeseme kuwa, hadi sasa hakuna mwanajeshi hata mmoja wa Ukraine aliyeweka chini silaha. Maelfu ya wanajeshi wa Russia waliojizatiti kwa mizinga na maroketi, wamesonga mbele kwa ajili ya kile kilichotajwa na maafisa wa Ukraine kuwa "vita ya kuidhibiti Donabas."
Wakati huo huo makamanda wa Ukraine wameapa kuwa, hawatasalimu amri huku Mkuu wa Majeshi ya Nchi hiyo akisema kuwa mapigano yalikuwa yakiendelea katika kiwanda cha chuma cha Azovstal. Amesema wanajeshi wa Russia wanashambulia karibu na mji wa Kaskazini Mashariki wa Kharkiv.
Juzi Jumanne Mykhailo Podolyak, Mshauri wa Rais wa Ukraine alisema kuwa, Russia inafanya mashambulizi katika kiwanda hicho cha chuma kwa kutumia mabomu yenye uwezo mkubwa wa kupenyeza ndani zaidi katika eneo lililokusudiwa. Kiwanda hicho cha chuma cha Azovstal ni ngome kuu iliyosalia huko Mariupol kwa upande wa jeshi la Ukraine.