75% ya Wamarekani wakatishwa tamaa na uchumi mbaya wa nchi yao
Aghalabu ya wananchi wa Marekani wamekatishwa tamaa na hali mbaya ya uchumi wa nchi hiyo.
Utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la habari la CBS News na YouGov unaonesha kuwa, asilimia 75 ya Wamarekani wanaitakidi kuwa, uchumi wa nchi yao unazidi kudorora.
Utafiti huo umesema robo tatu ya wananchi wa Marekani wanatiwa wasiwasi mkubwa na mdororo wa uchumi katika nchi hiyo, akthari yao wakishindwa kuhimili mfumko wa bei za bidhaa.
Mwezi uliopita wa Mei, Marekani ilitangaza kuwa uchumi wa nchi hiyo umeshuka kwa asilimia 0.4 katika robo ya kwanza ya mwaka huu 2022.
Janga la corona na mgogoro wa Ukraine vinatajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu za kuzorota kwa chumi nchi za Magharibi.
Wachumi wanasema wakati uchumi wa Ulaya unaathiriwa zaidi na mzozo wa Ukraine, uchumi wa Marekani unakabiliwa na kushuka kwa pato, mfumko wa bei pamoja na ukosefu wa ajira.
Vita na vikwazo ambavyo Russia imewekewa na Marekani, Ulaya na washirika wao vimeongeza uhaba wa chakula, nishati na madini muhimu, na kuvuruga biashara na kusababisha mfumuko wa juu wa bei katika nchi mbalimbali duniani.