Oct 13, 2022 10:51 UTC
  • WHO: Ulaya inaingia katika wimbi jipya la maambukizi ya COVID-19

Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Ulaya (ECDC) zimeonya kuhusu ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 katika nchi za Ulaya, katika kile kilichotajwa ni wimbi jipya la msambao wa maradhi hayo barani humo.

Hans Kluge, Mkurugenzi wa WHO barani Ulaya na Andrea Ammon, Mkurugenzi wa ECDC wamesema katika taarifa kuwa, "Ingawaje hatupo pahala tulipokuwa mwaka mmoja uliopita, lakini ni wazi kuwa janga la COVID-19 halijamalizika."

Taarifa hiyo ya pamoja imebainisha kuwa, "Kwa bahati mbaya tunaona dalili za ongezeko la maambukizi barani Ulaya, kuashiria kuwa wimbi jipya la msambao limeanza."

Takwimu za WHO zinaonesha kuwa, bara Ulaya ndilo eneo pekee lililonakili ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 kufikia mwishoni mwa wiki iliyomaizika Oktoba 2, likisajili ongezeko la asilimia 8 ikilinganishwa na wiki ya kabla yake.

Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Ulaya (ECDC) zimetahadharisha kuwa, mamilioni ya watu barani Ulaya hawajapiga chanjo dhidi ya COVID-19, huku zikiwatolewa mwito wa kuchanja wakati huu wanapojiandaa kupiga chanjo dhidi ya mafua ya msimu. 

Hivi karibuni, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) alionya kuwa, walimwengu hawapaswi kughafilika wala kuchukulia kama janga la COVID-19 limeisha duniani, na kwamba watu zaidi ya milioni moja wamefariki dunia kwa ugonjwa huo mwaka huu pekee.

Watu zaidi ya milioni 6.5 wameaga dunia kwa maradhi ya COVID-19 tangu kesi ya kwanza ya maambukizo ya virusi hivyo iliporipotiwa Disemba 31, 2019 katika jimbo la Wuhan nchini China. Akthari ya vifo na kesi za maradhi hayo ziliripotiwa Marekani na katika nchi za Ulaya.

Tags