PEC: Ulaya si salama kwa wanahabari, 37 wameuawa 2022
Shirika la kufuatilia masuala ya wanahabari la Press Emblem Campaign (PEC) limesema waandishi wa habari na wafanyakazi wengine katika sekta ya upashaji habari 115 wameuawa katika sehemu mbalimbali duniani mwaka huu, hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 45 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Ripoti ya shirika la PEC iliyotolewa jana Jumatano inaonesha kuwa, mauaji yaliyoshuhudiwa mwaka huu dhidi ya wanahabari ndiyo makubwa zaidi kuwahi kurekodiwa tokea mwaka 2018; huku Amerika ya Latini na Ulaya zikiongoza.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanahabari 39 wameuawa katika eneo la Amerika ya Latini tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, huku bara Ulaya likishika nafasi ya kwa pili kwa kusajili vifo 37.
Press Emblem Campaign (PEC) imesema, bara Asia limenakili vifo 30 vya waandishi wa habari mwaka huu, bara Afrika 7, huku Amerika Kaskani ikirekodi vifo viwili.
Kwa mujibu wa shirika hilo, Ulaya imeshuhudiwa ongezeko kubwa la ukosefu wa usalama kwa wanahabari, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa ongezeko hilo tokea vita vya Yugoslavia ya zamani baina ya mwaka 1992 na 1999.
Wakati huohuo, Jumuiya ya Maripota Wasio na Mipaka (RSF) imesema wanahabari 533 wamekamatwa na kuzuiliwa katika sehemu mbalimbali duniani mwaka huu, ongezeko la asilimia 13.4 ukilinganisha na takwimu za mwaka jana.