"Marekani haiwezi kustahamili sauti ya vyombo huru vya habari"
Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) ametoa radiamali yake kwa hatua ya karibuni ya Marekani ya kuviwekea vikwazo vyombo vitatu vya habari vya Iran ikiwemo kanali ya Press TV na kusisitiza kuwa, "Marekani kamwe haiwezi kuvumulia sauti ya vyombo huru vya habari."
Dakta Peyman Jebelli amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Tasnim na kueleza kuwa, kuviwekea vikwazo vyombo vya habari si kitu kipya kwa Marekani, na kwamba vikwazo hivyo ni aina fulani ya udikteta wa kimataifa wa vyombo vya habari.
Amesema Marekani katika miaka ya hivi karibuni imetumia kila njia ijuayo kuvibana na kuvishinikiza vyombo huru vya habari katika hali ambayo, inadai kuwa inaheshimu uhuru wa vyombo hivyo.
Jebelli amesisitiza kuwa, vyombo vya habari vina nafasi muhimu ya kufichua njama za kuzusha fitina za maadui na mipango yao yenye lengo la kuzipotosha fikra za walio wengi ulimwenguni.
Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, "Kile ambacho kinafunzwa katika Vyuo Vikuu vya Magharibi juu ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya madai ni madai hewa tu."
Dakta Jebelli amesema hayo baada ya Marekani na nchi kadhaa za Ulaya kutangaza vikwazo dhidi ya maafisa na wahariri wakurugenzi wa vyombo vya Jamhuri ya Kiislamu, mbali na kutoa matamshi ya uingiliaji dhidi ya taifa hili.
Marekani inajulikana kama nchi inayoongoza duniani kwa uwekaji vikwazo, ikiwa na rekodi ndefu zaidi ya kuziwekea nchi zingine kila aina ya vikwazo kwa ajili ya kufanikisha malengo na maslahi yake.