Kiongozi Muadhamu: Hatusubiri idhini ya yeyote katika kurutubisha madini ya urani
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Iran haingojei ruhusa ya mtu yeyote ili kurutubisha madini ya urani na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ina sera zake.
Ayatullah Seyyed Ali Khamenei amesema hayo leo katika Husseiniya ya Imam Khomeini (ra) kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja tangu kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi pamoja na maafisa wa serikali aliokuwa amefuatana nao akiwemo Hussein Amir-Abdollahian aliyekuwa waziri wake wa mashauri ya kigeni na kueleza kwamba, hatuamini kwamba mazungumzo ya Iran na Marekani yatafikia natija.
Akimuelezea shahidi Raisi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Shahidi Raisi hakujiona kuwa ni bora kuliko raia; bali alijiona kuwa katika kiwango sawa na watu wengine, mithili ya watu wengine, na hata mdogo kuliko watu wengine.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Tulizungumzia kuhusu mazungumzo, na ningependa kutoa onyo kwa upande wa pili: Upande wa Marekani ambao unashiriki katika mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja, lazima uache kutoa kauli za kipumbavu."

Ayatullah Khamenei amesema: Upande mwingine [wa mazungumzo] unasema kwa ujeuri kabisa kwamba, hatutaruhusu Iran kurutubisha madini ya urani. Hakuna anayesubiri ruhusa kutoka upande wowote." Jamhuri ya Kiislamu ina sera na misingi na inafuata sera yake yenyewe.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: "Nitawaeleza wananchi wa Iran katika tukio na mnasaba mwingine maudhui ya kurutubisha madini ya urani, na kwa nini Wamagharibi, na hasa Wamarekani wanashikilia sana kuzuia urutubishaji nchini Iran. Nitashughulikia masuala haya, Mwenyezi Mungu akipenda, katika tukio la baadaye ili wananchi wa Iran wajue nini makusudio ya upande mwingine [wa mazungumzo]."