Wanaharakati wa Kenya kuishtaki serikali ya Tanzania kwa ukiukaji wa haki
(last modified Tue, 20 May 2025 13:16:47 GMT )
May 20, 2025 13:16 UTC
  • Wanaharakati wa Kenya kuishtaki serikali ya Tanzania kwa ukiukaji wa haki

Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Kenya wanapanga kwenda mahakamani kuishtaki serikali ya Tanzania, kwa kile wanasema imekiuka haki za kibinadamu.

Wanaharakati hao wa Kenya wanasema wataishtaki serikali ya Tanzania kufuatia kuwakamata na kuwafukuza nchini humo wanaharakati waliotaka kuhudhuria kesi ya mwanasiasa za upinzani Tundu Lissu.

Akizungumza baada ya kurudishwa nyumbani, mkurugenzi wa shirika la Vocal Afrika, Khalid Hassan, akiwa sambamba na jaji mkuu wa zamani wa Kenya, Willy Mutunga na mwanaharakati Hanifa Adan, amesema wanatafuta ushauri wa kisheria.

“Tuna nia ya kuweza kulifikisha suala hili mahakamani ili mambo kama haya yasiweze kujirudia tena katika mataifa ya Afrika Mashariki.”  Alisema Khalid Hassan.

Kufukuzwa kwa wanaharakati hao, kulikuja siku moja kupita tangu idara za usalama katka uwanja wa ndege wa Julius Nyerere zimkamate waziri wa zamani wa sheria wa Kenya, Martha Karua, pamoja na wanasheria wengine wawili na kuwafukuza.

 

Mwanasiasa maarufu wa Kenya Martha Karua ambaye pia ni mwanasheria anayewakilisha vigogo wa upinzani wanaokabiliwa na kesi katika mataifa jirani, juzi alikamatwa nchini Tanzania katika uwanja wa ndege na kurejeshwa nchini Kenya baada ya kushikiliwa kwa masaa kadhaa.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa onyo kali kwa wanaharakati kutoka nchi jirani kuacha kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania, akisisitiza kuwa taifa hilo haliwezi kuwa “shamba la bibi” ambapo kila mtu anaingia na kufanya apendavyo.

Wakati huo huo, Issac msemaji wa serikali ya Kenya amesema kuwa kuondoshwa kwa Martha Karua nchini Tanzania hakutavuruga uhusiano wa kidiplomasia kati ya Kenya na Tanzania.