Jeshi la Sudan: Tunakaribia kudhibiti tena Khartoum
(last modified Wed, 21 May 2025 02:26:52 GMT )
May 21, 2025 02:26 UTC
  • Jeshi la Sudan: Tunakaribia kudhibiti tena Khartoum

Jeshi la Sudan lilisema jana Jumanne kwamba, vikosi vyake vinakaribia "kusafisha kabisa" Jimbo la Khartoum toka mikononi mwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

Msemaji wa Jeshi la Sudan, Nabil Abdullah amesema hayo katika taarifa na kuongezan kuwa, "Vikosi vyetu vinaendelea kuwaangamiza wanamgambo wa RSF kusini na magharibi mwa Omdurman."

Amesema wanajeshi wa Sudan pia wanaendelea 'kulisafisha' eneo la Salha, kusini mwa Omdurman na viunga vyake yake, baada ya kutoa vipigo vikali kwa wanamgambo wa RSF.

"Tunaendelea na operesheni yetu kubwa na tunakaribia kulisafisha jimbo lote la Khartoum," ameongeza msemaji wa jeshi la Sudan.

Hakuna taarifa iliyotolewa kufikia sasa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kufikia sasa juu ya taarifa hiyo ya jeshi la Sudan.

Kabla ya hapo, Jeshi la Sudan lilitangaza habari ya kufanikiwa kutwaa tena udhibiti wa eneo muhimu la kistratajia la Attrun huko Darfur Kaskazini kutoka kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

Jeshi la Sudan limekuwa likipambana na waasi wa RSF tangu Aprili 2023, na vita hivyo vimepelekea vifo vya maelfu ya watu na kusukuma Sudan katika moja ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani. 

Zaidi ya watu 20,000 wameuawa na milioni 15 wamekimbia makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa na mamlaka za mitaa. Utafiti wa baadhi ya taasisi huru hata hivyo unaweka idadi ya vifo kuwa karibu 130,000.