AU yapongeza kuteuliwa Waziri Mkuu raia nchini Sudan
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) Mahmoud Ali Youssouf amepoongeza kuteuliwa Kamil Idris kwa Waziri Mkuu mpya wa Sudan, na kusema kuwa hiyo ni hatua ya kuelekea kwenye utawala jumuishi katika nchi hiyo inayoendelea kuteseka kwa migogoro.
Katika taarifa yake ya jana, Youssouf amesema kuwa, uteuzi huo utachangia pakubwa katika juhudi zinazoendelea za kurejesha utulivu na utawala wa kidemokrasia nchini Sudan.
Hatua hiyo inafuatia agizo la kikatiba lililotolewa Jumatatu na Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Sudan ambaye pia ni mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye amemteua rasmi Kamil Idris kushika wadhifa huo.
Akitilia mkazo kuwa tayari Umoja wa Afrika kuiunga mkono Sudan katika kipindi hiki cha mpito wa kisiasa, Youssouf ametoa mwito kwa pande zote husika kuzidisha juhudi zao kuelekea mchakato wa amani, unaoongozwa na raia, shirikishi na unaoakisi matarajio ya watu wa Sudan.
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wenye wanachama 55 amesisitiza pia kwamba umoja huo una dhamira thabiti ya kuleta utulivu nchini Sudan na kutafuta suluhu ya kudumu ya kisiasa ambayo italinda amani, maendeleo na utawala wa kidemokrasia kwa Wasudan wote.
Uteuzi wa Idris umekuja karibu wiki tatu baada ya al-Burhan kumteua Dafallah al-Haj Ali kuwa kaimu waziri mkuu na waziri wa maswala ya baraza la mawaziri. Nafasi hiyo imekuwa wazi tangu kiongozi wa kiraia Abdalla Hamdok alipojiuzulu mwezi Januari 2022 kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Al-Burhan mwezi Oktoba 2021.
Kamil Idris ni mtaalamu wa sheria, hapo awali aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Haki Miliki Duniani na Katibu Mkuu wa Muungano wa Kimataifa wa Kulinda Aina Mpya za Mimea.