Wanajeshi 7 wa Israel waangamizwa Khan Yunis
Wanajeshi wasiopungua 7 wa utawala haramu wa Israel wameangamizwa na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia shambulio la kuvizia la vikosi vya muqawama huko Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Jeshi la Israel limekiri kuuawa kwa wanajeshi wake saba katika mji wa Khan Yunis ulioko kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa Al-Mayadeen, jeshi la Israel lilikiri kuwa wanajeshi 7 waliuawa katika shambulio la kuvizia lililowekwa na vikosi vya muqawama.
Jeshi la Israel lilitangaza kuwa wanajeshi hao saba waliuawa siku ya Jumanne wakati wa mlipuko wa shehena ya kubebea silaha huko Khan Yunis, kusini mwa Gaza.
Jeshi la Israel pia limekiri kujeruhiwa kwa askari wake kadhaa na kutangaza kuwa hali ya baadhi yao ni mbaya.
Hapo awali vyombo vya habari vya Israel vilitangaza kuwa wanajeshi 4 wa Israel waliuawa na wengine 17 kujeruhiwa katika shambulizi la kuvizia huko Khan Yunis, baadhi yao wakiripotiwa kuwa katika hali mbaya.
Kulingana na takwimu za jeshi, idadi ya askari wake walioangamizwa tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza, Oktoba 7, 2023, sasa imeongezeka na kukaribia 1000.
Takwimu hizo zinajumuisha wanajeshi waliouawa katika Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi, Lebanon na ndani ya Israel.
Wapigania ukombozi wa Palestina wanasisitiza kwamba hasara ya vikosi vya utawala haramu wa Israel ni kubwa zaidi kuliko inayotangazwa.