Taifa Lenye Umoja
https://parstoday.ir/sw/news/event-i127658-taifa_lenye_umoja
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu chenye anuani isemayo “Taifa Lenye Umoja”. Katika kipindi hiki maalumu tunakusudia kuzungumzia na kujadili umoja na mshikamano wa Wairani mkabala na maadui katika matukio mbalimbali likiwemo hili la hivi karibuni la hujuma na mashambulio ya kijeshi ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Iran.
(last modified 2025-10-14T05:46:07+00:00 )
Jun 25, 2025 11:23 UTC
  •  Taifa Lenye Umoja

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu chenye anuani isemayo “Taifa Lenye Umoja”. Katika kipindi hiki maalumu tunakusudia kuzungumzia na kujadili umoja na mshikamano wa Wairani mkabala na maadui katika matukio mbalimbali likiwemo hili la hivi karibuni la hujuma na mashambulio ya kijeshi ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Iran.

 

Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo.

 

Ikiwa huniamini, angalia historia. Taifa la Iran daima limekuwa na umoja na mshikamano kwa hali zote.

Tangu zama za kale hadi sasa, Wairani daima wamekuwa pamoja, wenye mshikamano, wakihurumiana, na wameungana katika mizozo mbalimbali na kupitia misukosuko mingi, na hii ndiyo siri ya ushindi wa Iran na Wairani.

Tangu saa za mwanzo kabisa za uvamizi wa utawala wa Kizayuni katika ardhi ya Iran, alfajiri ya Juni 13, taifa kubwa na tukufu la Iran limesimama bega kwa bega na mshikamano dhidi ya utawala huo wa kihalifu.

Adui amekuwa akifikiria kwa muda mrefu kwamba inawezekana kuharibu uhusiano na umoja huu wa kina kati ya watu wa Iran, lakini uhusiano kati ya Iran na Wairani ni mkubwa sana kuweza kuharibiwa na njama za maadui wahalifu.

Katika kurasa nyinginezo za historia, madhihirisho ya huruma na mshikamano wa Iran dhidi ya hujuma na uvamizi wa utawala wa Kizayuni yamerekodiwa, na kwa mara nyingine tena ulimwengu unashuhudia umoja na uelewa wa watu wa Iran.

Hapana shaka kuwa, ufunguo wa mafanikio na ushindi katika jamii yoyote ile ni umoja na mshikamano. Chambiliecho methali ya Kiswahili: Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Suala hili muhimu limekuwa likizingatiwa mno na Wairani kwa muda mrefu. Kwa hivyo, katika historia na katika hali ngumu zaidi, Wairani daima wamesimama pamoja na kuwa na umoja wenye nguvu.

Kwa kuipitia historia, tunaona kwamba tangu maelfu ya miaka iliyopita hadi leo hii, Wairani wamepigania ardhi yao, na juhudi hizi zimefanyika chini ya kivuli cha umoja na mshikamano wa wananchi wa Iran.

Kwa miaka mingi, maadui wa Iran wamekuwa wakijaribu kwa njia mbalimbali kuharibu umoja na mshikamano baina ya wananchi wa Iran, lakini siku baada ya siku na dakika baada ya dakika, mnyororo wa umoja na mshikamano unazidi kuimarika.

 

Utawala bandia wa Kizayuni ulifikiri kwamba kwa kuivamia ardhi ya Iran, uzi wa umoja kati ya Wairani ungekatika, lakini kinachoonekana hivi sasa ni mshikamano na si mfarakano.

Ndio, watu wa ardhi hii ni watoto wa hamasa na walinzi wa damu za mashahidi. Watu wa Iran, kwa umoja na mshikamano, ndio walinzi wa nchi na wanasimama kwa nguvu dhidi ya maadui wote wa ardhi ya nchi hii.

Taifa lenye ghera la Iran, likiwa na umoja wake, lugha moja, huruma na mshikamano, limewapigisha magoti maadui madhalili kama vile Marekani, utawala wa Kizayuni na nchi za Magharibi na Ulaya.

Hivi sasa, dunia nzima inashuhudia umoja kati ya wananchi na mfumo mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika hali ambayo nchi ya Iran ilishambuliwa na adui Mzayuni na kudhuriwa wanawake na watoto wasio na hatia, wananchi watukufu wa Iran wameunda mandhari ya kipekee ya mshikamano na umoja huku wakipaza sauti moja:

"Katika siku ambazo utawala dhalimu wa Kizayuni umekiuka ardhi ya Iran, sisi, taifa kubwa la Iran, tunasimama pamoja, kwa ajili ya nchi yetu, kwa ajili ya watu wetu, mpaka katika siku ambayo amani itarejea katika ardhi yetu tunayoipenda."

 

Wapenzi wasikilizaji mnaendelea kutegea sikio Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kipindi hewani ni makala maalumu ya Taifa Lenye Umoja.

Moja ya masuala muhimu yanayopaswa kutajwa katika moyo wa hujuma na uvamizi wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Iran ni umoja wa kitaifa baina ya wananchi wa Iran.

Taifa kubwa la Iran katika kukabiliana na tabia chafu ya adui, lilionyesha muqawama wa kitaifa usio na kifani na, bila shaka wa kupongezwa.

Maadui wa Iran na vyombo vya habari vya uadui vimekuwa na vinajaribu kupunguza uelewa huu, lakini umoja wa kipekee wa kitaifa wa Wairani na uhusiano wa kina ambao umeanzishwa kati ya wasomi wa Iran, watu, maafisa, vikosi vya usalama na kiintelijensia  vimeonyesha moja ya matukio mazuri zaidi katika historia ya kisasa ya Iran mbele ya macho ya ulimwengu.

Hivi leo adui anatumia zana zote alizonazo, kuanzia uwezo wa kijeshi hadi vyombo vya habari dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini hakuna zana yoyote ya adui yenye uwezo wa kukabiliana na umoja na mshikamano wa taifa kubwa la Iran.

Inafaa katika sehemu hii kuashiria maneno ya Kiongozi wa Mapinduzi, Ayatullah Khamenei, ambaye alisema:

"Ishara ya nguvu ya taifa la Iran ni kuushinda mlolongo wa uhasama mtawalia uliodumu kwa miongo kadhaa. Katika kukabiliana na mapinduzi, vikwazo, mashinikizo ya kisiasa, njama za kiusalama na uvamizi wa vyombo vya habari."

Hujuma hii ya vyombo vya habari ambayo wameanzisha ya chuki dhidi ya Iran (Iranophobia) na chuki dhidi ya mapinduzi haijawahi kutokea ulimwenguni. Kitu kama hiki katu hakijawahi kutokea ... Je! unajua nchi au mapinduzi yoyote ambayo yameweza kustahimili mapigo ya nchi zenye nguvu zaidi ulimwenguni kwa miaka mingi, ambayo imesimama kidete na kutopiga magoti?..."

Hapana shaka kuwa, moja ya sababu muhimu zaidi za muqawama wa Iran dhidi ya njama za maadui ni umoja na mshikamano uliopo baina ya wananchi wa Iran.

Katika kivuli cha umoja na maelewano hayo, hivi leo taifa lenye ghera la Iran linasimama kwa ujasiri, ushujaa na uthabiti wa hali ya juu kabisa dhidi ya utawala dhalimu wa Kizayuni na litapinga hadi kuangamizwa kikamilifu utawala huo muovu.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulifanya kosa kubwa kuivamia ardhi ya Iran bila ya kujua uwezo wa kijeshi, ulinzi na usalama wa Iran. Kwa upande mwingine, utawala huo bandia na mtenda jinai haukuwa na ufahamu wowote kuhusu jamii ya Iran na haukujua kwamba Iran ni miongoni mwa nchi chache za eneo ambazo hisia za uzalendo na utambulisho wa kitaifa ni zenye nguvu na dhahiri.

Wakati adui anapoishambulia ardhi ya Iran, huenea hisia ya kawaida miongoni mwa watu wa Iran katika kukabiliana na adui. Hisia hii ya kawaida na iliyoenea inazifunga nyoyo na nafsi za Wairani pamoja na kuleta umoja, na umoja huu ni kizuizi na kinga kubwa dhidi ya adui.

Tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran hadi hivi sasa, maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima wamekuwa na wanajaribu kuharibu kizuizi  na kinga hiyo yenye nguvu yaani umoja na mshikamano wa kitaifa.

Maadui wanaoichukulia Iran iliyoungana, iliyo huru na iliyo na umoja na mshikamano kuwa kikwazo cha malengo yao maovu na ya kishetani, wanapaza sauti mfarakano na kusisitiza jambo hilo, na kujaribu kufikia malengo yao maovu kwa kuleta mifarakano na migawanyiko kati ya wananchi wa Iran, lakini taifa kubwa la Iran limesimama kwa akili na uwezo mkubwa dhidi ya silaha ya adui huyu.

Wananchi wa Iran kwa kuendelea kuwa watiifu kwa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena wamethibitisha kwamba muqawama huo ni wa ushindi na kwamba utawala dhalimu wa Kizayuni hautafaulu kuidhuru Iran na Wairani, bali utajiletea maangamizi yake yenyewe.

Wananchi wa Iran wameonyesha kuwa kila linapotajwa suala la kutetea nchi na usalama wa nchi kila mmoja yuko tayari kulifanyia kazi. Kama ambavyo walisimama dhidi ya uchokozi wa utawala wa Baath wa Iraq wakati wa vita vya kujihami kutakatifu vya miaka minane, leo pi wako tayari kutetea utu na uhuru wao na kusimama kidete dhidi ya utawala vamizi wa Israel na Marekani.

 

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki maalumu cha Taifa Lenye Umoja” umefikia tamati, basi hadi tutakapokutana tena katika kipindi kingine ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.

Asanteni na kwaherini.