Pakistan yaapa kulipiza kisasi dhidi ya Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i131902-pakistan_yaapa_kulipiza_kisasi_dhidi_ya_afghanistan
Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amelaani kitendo alichokiita ni cha uchokozi kutoka kwa nchi jirani ya Afghanistan.
(last modified 2025-10-12T10:56:57+00:00 )
Oct 12, 2025 10:56 UTC
  • Pakistan yaapa kulipiza kisasi dhidi ya Afghanistan

Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amelaani kitendo alichokiita ni cha uchokozi kutoka kwa nchi jirani ya Afghanistan.

Shehbaz Sharif amesema kuwa, nchi yake itajibu vikali baada ya pande hizo mbili kushambuliana usiku kucha katika eneo la mpakani. Waziri Mkuu, wa Pakistan amelaumu mamlaka ya wanamgambo wa Taliban kwa kuruhusu ardhi yao kutumiwa na magaidi.

Kwa upande wa Afghanistan, msemaji mkuu wa serikali ya Taliban, Zabihullah Mujahid, amesema kuwa, vikosi vya Afghanistan vimekamata vituo 25 vya jeshi la Pakistan, wanajeshi 58 wa Pakistan wameuliwa na wengine 30 wamejeruhiwa katika oparesheni hiyo na kwamba hayo yalikuwa majibu ya ukiukaji wa mara kwa mara kwenye anga na ardhi yake unaofanywa na Pakistan.

Hayo yanajiri baada ya mapigano makali kuzuka mpakani kati ya majeshi ya Afghanistan na Pakistan huku vikosi vya nchi hizo mbili vikishambuliana kwa kutumia silaha nzito.

Mapigano hayo yalipamba moto jana Jumamosi siku moja baada ya serikali ya muda ya Afghanistan inayoongozwa na Taliban kulituhumu jeshi la Pakistan kuwa lilikiuka anga ya mji mkuu Kabul siku ya Alkhamisi usiku na kuripua soko moja kwenye eneo la Margha lililoko katika jimbo la Paktika linalopakana na Pakistan.

Islamabad haikuthibitisha wala kukanusha kuwa ilihusika na mashambulizi hayo lakini ilisema itatumia kila njia kuwalinda raia wake kwa sababu imekuwa ikishuhudia ongezeko la ugaidi inaouhusisha na kundi ililolipiga marufuku la Tehreek-i-Taliban Pakistan (TTP) ambalo inadai wapiganaji wake wanapewa hifadhi na serikali ya Taliban na kusaidiwa pia na hasimu wake India.