Iran: Dunia iwe macho, isikubali Israel ikiuke usitishaji vita Gaza
Iran imesisitiza uungaji mkono wake usioyumba kwa juhudi zozote zinazolenga kukomesha mauaji na mauaji ya halaiki ya Israel huko Gaza, ikionya kuhusu historia ya utawala unaoikalia kwa mabavu Quds ya kukanyaga mikataba na makubaliano.
Katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari leo Jumatatu hapa Tehran, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei amesema takwa kuu la Tehran ni kukomesha jinai huko Gaza na mzingiro, pamoja na kupewa misaada ya kibinadamu Wapalestina wa eneo hilo lililoharibiwa na vita.
"Uzoefu katika eneo letu katika miongo michache iliyopita, ikiwa ni pamoja na utawala wa Kizayuni kukosa dhamira na kukiuka mara kwa mara makubaliano ya usitishaji vita nchini Lebanon, ambapo zaidi ya kesi 4,500 za ukiukaji wa usitishaji mapigano zimenakiliwa.
Amebainisha kuwa, makubaliano ya hivi karibuni ya usitishaji vita kati ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas na Israel yalifikiwa baada ya siku 700 za mauaji ya halaiki ya utawala huo ghasibu huko Gaza na kuwatwisha Wapalestina njaa.
"Iran imetangaza wazi msimamo wake kuhusu makubaliano hayo ambayo yanalenga kukomesha mashambulizi ya utawala wa Israel," amesema.
Hali kadhalika, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema uamuzi wa Iran wa kutohudhuria mkutano wa kilele wa Sharm El-Sheikh kuhusu Gaza ulifanywa kufuatia mashauriano ya wataalamu, na kusisitiza kwamba kutokuwepo kwa Jamhuri ya Kiislamu huko Misri hakumaanishi ukosefu wa ushawishi katika maendeleo ya kieneo au kimataifa.
Akizungumzia matamshi ya Rais Vladmir Putin wa Russia kuhusiana na ujumbe kutoka kwa utawala wa Israel kwa Iran, Baghaei alibainisha kuwa Tehran inasikiliza mapendekezo ya mataifa marafiki lakini bado iko macho kabisa juu ya matukio ya kieneo, akisisitiza kwamba kutokana na historia ya hadaa, na udanganyifu ya utawala wa Kizayuni, "Iran itaendelea kuwa macho katika ngazi zote."