Mali yajibu mapigo, yawawekea Wamarekani vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131942-mali_yajibu_mapigo_yawawekea_wamarekani_vikwazo
Serikali ya Mali imeweka masharti ya bondi ya viza kwa raia wa Marekani, ili kulipiza kisasi cha uamuzi wa Washington wa kuwawekea vikwazo vya usafiri raia wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
(last modified 2025-10-13T11:29:46+00:00 )
Oct 13, 2025 11:29 UTC
  • Mali yajibu mapigo, yawawekea Wamarekani vikwazo

Serikali ya Mali imeweka masharti ya bondi ya viza kwa raia wa Marekani, ili kulipiza kisasi cha uamuzi wa Washington wa kuwawekea vikwazo vya usafiri raia wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Marekani imewataka waombaji wote wa viza vya biashara au watalii nchini Mali kulipa bondi za kati ya dola 5,000 na $10,000 kuanzia Oktoba 23.

Katika taarifa yake Jumapili, Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali ilikosoa "uamuzi huo wa upande mmoja" na kusema unakiuka makubaliano ya nchi mbili ya 2005, ambayo yaliruhusu viza za muda mrefu na za kuingia mara nyingi kati ya nchi hizo mbili.

"Katika kutekeleza kanuni ya kujibu mapigo, Mali imeamua kuanzisha mpango wa viza sawa na uliowekwa na Marekani. Masharti na mahitaji sawa na yale yanayotumika kwa raia wa Mali yatatumika pia kwa raia wa Marekani wanaotaka kuitembelea nchi hii," wizara hiyo imesema.

Mali ni mojawapo ya nchi tano za Kiafrika ambazo Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliorodhesha Jumatano iliyopita, kwa mpango wa majaribio wa bondi ya mwaka mzima, pamoja na Mauritania, Sao Tome na Principe, Tanzania, na Gambia.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imedai kuwa, mpango huo unakusudia kupunguza viwango vya juu vya wahamiaji wanaoishi kwa muda mrefu kupindukia nchini humo.

Ijumaa iliyopita, Ubalozi wa Marekani nchini Burkina Faso ulitangaza kuwa umesitisha huduma zote za viza baada ya taifa hilo la Afrika kukataa matakwa ya Washington ya kuwakubali watu wanaofukuzwa kutoka nchi ya tatu.