Wanajeshi wa Madagascar waungana na waandamanaji wanaoipinga serikali katika mji mkuu
Baadhi ya makundi ya wanajeshi wa Madagascar yamekaidi amri na kuungana na maelfu ya waandamanaji wanaoipinga serikali, ambao wamekusanyika katika mji mkuu, Antananarivo, huku maandamano ya kupinga utawala wa Rais Andry Rajoelina yakizidi kupamba moto.
Waandamanaji wanaoongozwa na vijana walimiminika katika Medani ya Mei 13 jana Jumamosi kwa mara ya kwanza katika moja ya mikusanyiko mikubwa zaidi tangu lilipoanza vuguvugu la maandamano ya upinzani katika kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi mnamo Septemba 25, ambalo lilichochewa na kile kinachojulikana kama maandamano ya Gen Z yaliyozuka katika nchi za Kenya na Nepal.
Baada ya polisi kutumia magurunedi na mabomu ya kutoa machozi kujaribu kuwatawanya waandamanaji, askari wa jeshi walifika eneo la tukio na kupokelewa kwa shangwe.
Katika mkutano uliofanyika hapo kabla kwenye kambi ya jeshi nje kidogo ya jiji, wanajeshi wa kitengo cha wenye vipawa cha CAPSAT, ambacho kilikuwa na jukumu muhimu katika kuibuka kisiasa kwa rais Rajoelina mnamo mwaka 2009, walitoa wito nadra kushuhudiwa wa kuwepo mshikamano huku waandamanaji wakimtaka kiongozi huyo ajiuzulu.
"Wacha tuunganishe nguvu, wanajeshi, askari na polisi, na kukataa kulipwa kuwapiga risasi marafiki zetu, kaka zetu na dada zetu," walitamka askari hao waliokuwa kwenye kambi iliyoko wilayani Soanierana kupitia mkanda wa video uliowekwa kwenye mtandao wa kijamii.
Aidha, walitoa wito kwa askari katika uwanja wa ndege kuzuia ndege zote zisiruke na kwa wale walioko katika kambi nyingine wakatae maagizo ya kuwapiga risasi marafiki zao.
“Fungeni mageti, na mngojee maagizo yetu,” waliagiza wanajeshi hao na kuendelea kusema: "msitii amri kutoka kwa wakubwa zenu. Waelekezeeni silaha wale wanaokuamrisheni muwafyatulie risasi wenzenu kwa sababu tukifa, wao hawatatutunzia familia zetu".
Maandamano ya jana Jumamosi yalikuwa makubwa zaidi kushuhudiwa katika siku kadhaa za vuguvugu lililoongozwa na vijana, ambalo lilichochewa na hasira juu ya uhaba wa umeme na maji na kuibuka kuwa kampeni pana ya kupinga serikali.../