Ansarullah yaipa muda Israel kuhakikisha inatekeleza kikamilifu usitishaji vita Ghaza
Kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa harakati ya Ansarullah ya Yemen ameupa utawala wa Kizayuini muda maalumu wa kuhakikisha unaheshimu na kutekeleza makubaliano ya kusimamisha vita vinginevyo Yemen itaanzisha tena operesheni za kijeshi dhidi ya Israel.
Shirika la Habari la Fars limemnukuu "Hizam al-Assad" mjumbe mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah akisema hayo jana Jumapili na kusisitiza kuwa, kama Israel itaheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano huko Ghaza, Ansarullah nayo itasimamisha mashambulizi yake lakini kama Tel Aviv itakiuka makubaliano hayo, itambue kuwa jibu la Ansarullah litakuwa kali zaidi na la kuumiza zaidi.
Vilevile amesema, usitishaji wowote wa operesheni za Yemen dhidi ya Israel unategemea mienendo ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza. Ikumbukwe kuwa Yemen ilikuwa ni kambi nyingine imara ya vita dhidi ya Israel baada ya utawala wa Kizayuni kuanzisha mashambulizi ya kikatili dhidi ya Ukanda wa Ghaza tarehe 7 Oktoba 2023.
Yemen imefanya imefanya mashambulizi mengi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel tangu kuanza vita hivyo. Mashambulizi hayo yote yalifanywa na Yemen ili kuwaunga mkono Wapalestina na ili kuishinikiza Tel Aviv ikomeshe jinai zake kwenye Ukanda wa Ghaza iliouzingira kila upande.
Mengi ya mashambulio ya Yemen yalilenga maeneo ya kusini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni hasa eneo la Eilat, lakini baadhi ya droni na makombora yalikuwa yanapiga ndani zaidi ikiwa ni pamoja na Tel Aviv na hasa Uwanja wa Ndege wa Ben-Gurion.
Mashambulizi hayo yalikuuwa ni shinikizo kubwa la kiusalama kwa Israel na hata mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Yemen hayakulizuia taifa hilo shujaa kuitia adabu Israel.