Wazayuni wakiri kushindwa kuivunja na kuipokonya silaha HAMAS
Duru za habari za utawala wa Kizayuni wa Israel zimekiri kwamba vita vya Ghaza vimeisha na Hamas imepata mafanikio mengi kiasi kwamba licha ya kupita miaka miwili ya mashambulizi ya kila upande lakini Wazayuni wameshindwa kuivunja harakati hiyo kama ambavyo wameshindwa pia kuipokonya silaha.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, makubaliano ya kusitisha mapigano yamefikiwa huko Ghaza huku vyombo vya habari vya Kizayuni vikikiri kuwa jeshi la Israel limeshindwa kufikia malengo yake. Mtandao Kizayuni wa "I-24" umekiri kwamba, vita vimeshaisha tena Ghaza na Hamas imepata mafanikio mengi.
Duru za ndani ya Palestina ziliripoti jana kwamba makumi ya maelfu ya wakimbizi wa Palestina wameanza kurejea kwenye maeneo yao baada ya kutangazwa kusimishwa vita Ghaza. Waandishi wa habari wameripoti kuwa, Wapalestina waliorejea kwenye maeneo yao wamekumbana na uharibifu mkubwa sana wa nyumba na vitongoji vyao, kwani Israel imeteketeza kikatili na kila kitu kwenye sehemu kubwa za Ukanda wa Ghaza.
Kurejea Wapalestina kwenye maeneo yao ni hatua ya kwanza ya utekelezaji wa usitishaji mapigano ambao pia uliidhinishwa na baraza la mawaziri la Israel Ijumaa asubuhi. Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya siku nne za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Israel na Hamas huko Sharm el-Sheikh, Misri, yaliyopatanishwa na Ankara, Cairo, na Doha, na kusimamiwa na Marekani. Yanajumuisha kuachiliwa huru baadhi ya mateka wa Israel kwa kubadilishana mateka wa Palestina.
Mtandao Kizayuni wa "I-24" umekiri kuwa, Hamas bado ni taasisi yenye nguvu katika Ukanda wa Ghaza, haijavunjwa na wala haijapokonywa silaha. Chombo hicho cha habari cha Kizayuni kimedai kwamba Hamas iko mbioni kurejesha udhibiti kamili wa maeneo ya Ukanda wa Ghaza.