Maelfu ya Wapalestina waendelea kurejea Gaza baada ya vita kusitishwa
Maelfu ya raia wa Palestina waliokimbia makazi yao kufuatia mashambulio ya utawala wa kizayuni wa Israel wanaendelea kurejea kaskazini mwa mji wa Gaza kufuatia makubaliano ya usitishaji wa mapigano yaliyofikiwa wiki hii.
Makubaliano hayo yameleta matumaini kwamba, huenda mwafaka wa kudumu ukapatikana.
Ripoti zinasema kuwa, msururu mkubwa wa watu wakisafiri kwa miguu kuelekea kaskazini, umeonekana wakipitia barabara ya pwani kando ya fukwe kuelekea Jiji la Gaza, eneo kubwa zaidi la nchi kavu katika ukanda huo.
Wapalestina 200,000 wamekwisha rejea kaskazini mwa Gaza tangu usitishaji mapigano ulipoanza kutekelezwa.
Wakati huo huo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina, HAMAS pamoja na makundi mengine washirika ya Muqawama wa Palestina yamesisitiza kuwa uamuzi wowote kuhusu utawala wa baadaye wa Ghaza ni "suala la ndani la Palestina" na kupinga vikali eneo hilo kutawaliwa na kusimamiwa na maajinabi.
Bado haijafahamika kama mrengo wa Fat-h unaoshikilia hatamu za uongozi wa Mamlaka ya Palestina umekubali kuwa sehemu ya mkutano huo au la.
Mpango wa vipengele 20 uliopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump kwa ajili ya Ghaza unajumuisha kuundwa chombo kipya cha kimataifa, kilichopewa jina la "Bodi ya Amani", ambacho kitakuwa na jukumu la kusimamia mamlaka ya muda ya wateknokrati ya kuitawala Ghaza.
Kwa mujibu wa mpango huo, Trump mwenyewe amepangwa kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo, itakayomjumuisha pia waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair.