Vipengee muhimu vya makubaliano ya usitishaji vita Gaza
Utawala unaoukalia kwa mabavu Palestina na Hamas hatimaye wamefikia maelewano juu ya kutekeleza awamu ya kwanza ya usitishaji vita huko Gaza.
Makubaliano hayo yanaahidi kumalizika umwagaji damu. Mbali na kusitishwa vita huko Gaza vipengee vingine vya makubaliano hayo ni kubadilishana wafungwa 20 wa Israel mkabala wa wafungwa zaidi ya 2,000 wa Kipalestina. Aidha pande mbili zimekubalian kuruuhusiwa kuingia Gaza mamia ya malori ya misaada ya kibinadamu, na kurejea kwa wakimbizi.
Gazeti la Al-Arabi Al-Jadeed limechapisha ripoti kuhusu vipengele muhimu vya mkataba huo, na kuandika kuwa, kwa mujibu wa taarifa ilizozipata, makubaliano hayo yalipangwa kutiwa saini rasmi mjini Cairo jana Alkhamisi.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Israel imeahidi kuwaachia zaidi ya wafungwa 2,000 wa Kipalestina, wakiwemo 250 wanaotumikia vifungo vya maisha na 1,700 ambao wamezuiliwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Makubaliano hayo yanajumuisha pia kuingia kwa angalau malori 400 ya misaada kwa siku katika Ukanda wa Gaza katika siku tano za kwanza baada ya kusitishwa kwa mapigano. Kiwango hiki kitaongezeka katika siku zijazo. Aidha wakimbizi wa Kipalestina kutoka kusini mwa Ukanda wa Gaza wataruhusiwa kurejea katika mji wa Gaza na maeneo ya kaskazini.
Katika taarifa yake, harakati ya Hamas imemtaka Rais Donald Trump wa Marekani kuulazimisha utawala ghasibu wa Israel kutekeleza kikamilifu makubaliano hayo na kujiepusha na kusitasita au kutotekeleza.
Hamas sambamba na kuthibitisha kutiwa saini makubaliano ya kusimamisha vita imesema kwamba makubaliano hayo yatamaliza vita dhidi ya Gaza, wavamizi watatimuliwa na kutakuwa pia na kubadilishana mateka.