Maria Machado ashinda tuzo ya amani ya Nobel; Trump aambulia patupu
Mwanaharakati wa upinzani wa Venezuela María Corina Machado ameshinda Tuzo ya Amani ya Nobel 2025 kwa ujasiri wa kupigania demokrasia na uchaguzi huru licha ya vitisho. Kamati ya Nobel imemsifu kwa kuunganisha upinzani.
Tangazo hilo lilitolewa Ijumaa mjini Oslo, Norway, na Joergen Watne Frydnes, Mwenyekiti wa Kamati ya Nobel, aliyesema Machado “amekuwa kiungo muhimu cha umoja katika upinzani uliokuwa umepasuka – akisaidia kuunganisha wanasiasa na raia chini ya madai ya uchaguzi huru na utawala wa kidemokrasia.”
Kabla ya tangazo hilo, kulikuwa na tetesi kwamba tuzo hiyo ingeenda kwa Rais wa Marekani Donald Trump, kufuatia juhudi zake za kusitisha vita vya Gaza. Hata hivyo, wachambuzi walionya kuwa hatua hizo zilikuwa za hivi karibuni mno na haziwezi kufikia vigezo vya Nobel vinavyozingatia matokeo ya muda mrefu ya amani na ushirikiano wa kimataifa.
Alfred Nobel mkemia wa Sweden na mvumbuzi wa dynamite alikuwa na utajiri mkubwa na hakufikiri kuwa dynamite ingeweza kutumiwa vibaya, hivyo aliamua kutoa utajiri wake kama tuzo na zawadi. Alfred Nobel alifanya hivyo kwa lengo kwamba, tuzo hiyo itolewe kila mwaka kwa shakhsiya aliyefanya kazi kubwa ya thamani duniani katika masuala ya sayansi, fasihi na Amani.
Hata hivyo kinyume na matakwa yake, leo hii Tuzo ya Amani ya Nobel imechukua sura ya kisiasa na inatumiwa kama wenzo wa kutangaza na kueneza siasa za nchi za Magharibi duniani.