Trump amhutubu Netanyahu; Daima una misimamo hasi
Rais wa Marekani, Donald Trump amemkemea vikali Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa radimali yake hasi kwa jibu 'chanya' la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas kwa pendekezo la makubaliano ya kusitisha mapigano, ripoti imefichua.
Afisa mmoja wa Marekani ameambia chombo cha habari cha Axios leo Jumatatu kwamba, Trump aliripotiwa kumpigia simu Netanyahu siku ya Ijumaa ili kujadili jibu chanya la Hamas kwa pendekezo lake la kusitisha mapigano, ambalo alilizingatia kuwa habari njema.
Kiongozi huyo wa Israel, hata hivyo, alilipokea kwa njia tofauti, akimwambia Trump kwamba "hili si jambo la kusherehekea, na kwamba haimaanishi chochote." "Sijui ni kwa nini kila mara unakuwa (na misimamo) hasi. Huu ni ushindi. Upokee," Trump aliripotiwa kujibu.
Siku ya Jumamosi, wasaidizi wa Netanyahu walisisitiza kwamba misimamo yake "inalanda kabisa" na Trump. Hata hivyo, afisa huyo wa Marekani amesema majibizano wakati wa mawasiliano ya simu ya Ijumaa yalikuwa "ya kutatanisha," na kwamba Trump "alichukizwa" sana na Netanyahu.
Hamas ilithibitisha siku ya Ijumaa kuwa imekubali kuwaachilia mateka wa Israel lakini haikutaja kuwapokonya silaha. Trump ameitaka Israel kusitisha mashambulizi yake dhidi ya Gaza na kuitaka Hamas kuwaachilia mateka waliosalia ndani ya saa 72 baada ya Israel kusitisha mashambulizi yake ya kijeshi na kuwarejesha nyuma wanajeshi wake "kwenye mstari uliokubaliwa."
Israel imekubali kubadilishana wafungwa lakini haijajibu rasmi matakwa ya Trump ya kusitisha mashambulizi yake katika eneo lililozingirwa.
Hamas na utawala wa Israel wameratibiwa kuanza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya kusitisha mapigano nchini Misri siku ya Jumatatu.