Serikali ya Sudan: Waasi wa RSF wameua raia 57 wengine El Fasher
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131920-serikali_ya_sudan_waasi_wa_rsf_wameua_raia_57_wengine_el_fasher
Serikali ya Sudan imetangaza kwamba shambulizi la droni na ndege zisizo na rubani za Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF limeua raia 57 katika makazi yao ya muda ya mji wa El Fasher wa magharibi mwa Sudan.
(last modified 2025-10-13T02:27:56+00:00 )
Oct 13, 2025 02:27 UTC
  • Serikali ya Sudan: Waasi wa RSF wameua raia 57 wengine El Fasher

Serikali ya Sudan imetangaza kwamba shambulizi la droni na ndege zisizo na rubani za Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF limeua raia 57 katika makazi yao ya muda ya mji wa El Fasher wa magharibi mwa Sudan.

Sehemu moja ya taarifa ya serikali ya Sudan imesema: "Kama sehemu ya mpango wake unaoendelea wa kuwaangamiza kwa wingi watu waliokimbia makazi yao na raia huko El Fasher, wanamgambo hao wa kigaidi wamefanya mauaji mengine, katika makazi ya Dar Al-Arqam huko El Fasher." 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan, watu waliouawa kwenye shambulio hilo ni pamoja na watoto 17, wanawake 22 na wazee 18.

Wizara hiyo imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza ipasavyo majukumu yake hasa azimio lake la kuitaka RSF iache kuuzingira mji wa El Fasher mara moja na kusitisha mashambulizi dhidi ya mji huo.

Pia imewataka wahusika wote wa kimataifa na kikanda kuchukua hatua madhubuti za kukomesha kupelekewa silaha wapiganaji wa RSF, kwawajibisha viongozi wake, na kuunga mkono juhudi za serikali ya Sudan za kumaliza mateso ya raia huko El Fasher na miji mingine iliyozingira au kukaliwa kwa mabavu na RSF.

Hadi tunaandaa taarifa hii, RSF ilikuwa bado haijatoa tamko lolote kuhusiana na madai hayo ya serikali ya Sudan.

Mapigano makali yamekuwa yakiendelea huko El Fasher tangu mwezi Mei 2024, kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na vikosi vya washirika wake kwa upande mmoja, na RSF kwa upande mwingine, huku mapigano yakiwa makali zaidi siku za hivi karibuni.

Mgogoro kati ya SAF na RSF, uliozuka mwezi Aprili 2023, umeshaua makumi ya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao, na hivyo kuzidisha mzozo wa kibinadamu nchini Sudan.