AU yataka pande hasimu Madagascar kustahamiliana na kufungua mlango wa mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131922-au_yataka_pande_hasimu_madagascar_kustahamiliana_na_kufungua_mlango_wa_mazungumzo
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) Mahmoud Ali Youssouf jana Jumapili alizitaka pande zinazozozana nchini Madagascar kujizuia na kuvulimiana ili kufungua mlango wa mazungumzo wa kutatuliwa kisiasa mvutano uliozuka nchini humo.
(last modified 2025-10-13T02:28:22+00:00 )
Oct 13, 2025 02:28 UTC
  • AU yataka pande hasimu Madagascar kustahamiliana na kufungua mlango wa mazungumzo

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) Mahmoud Ali Youssouf jana Jumapili alizitaka pande zinazozozana nchini Madagascar kujizuia na kuvulimiana ili kufungua mlango wa mazungumzo wa kutatuliwa kisiasa mvutano uliozuka nchini humo.

Katika taarifa yake, Youssouf amesema, anafuatilia kwa "wasiwasi mkubwa" matukio ya kisiasa na kiusalama nchini Magascar ambayo yanaambatana na harakati za jeshi na maandamano ya umma katika mji mkuu, Antananarivo.

Akikaribisha dhamira mpya ya serikali ya kufanya mazungumzo, Youssouf amezitaka pande zote za Madagascar, raia na wanajeshi, kuwa watulivu na wenye kuvumiliana na badala yake kipaumbele chao kiwe ni kutatua masuala yao kwa njia za amani.

Vilevile ametoa mwito kwa vyama vyote vya Madagascar kuchukua hatua za uwajibikaji na za kizalendo ili kulinda umoja, utulivu na amani, kwa kuheshimu katiba kikamilifu.

Mwenyekiti wa AUC pia amesisitizia haja ya kuzingatiwa haki za kimsingi na uhuru wa raia wote, akitilia mkazo kuheshimiwa kanuni zilizowekwa katika mkataba wa bara la  Afrika wa Demokrasia, Uchaguzi na Utawala.

Wiki iliyopita, Rais wa Madagascar Andry Rajoelina alimteua Ruphin Fortunat Dimbisoa Zafisambo kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo, wiki moja baada ya kuivunja serikali huku kukiwa na maandamano makubwa. Rajoelina alisema kuwa, waziri mkuu mpya lazima awe na uwezo wa kurejesha utulivu na imani ya wawananchi, kupitia kuboresha hali ya maisha na kuendeleza vipaumbele muhimu vya kitaifa.

Waandamanaji wanaoongozwa na vijana walimiminika katika Medani ya Mei 13 juzi Jumamosi kwa mara ya kwanza katika moja ya mikusanyiko mikubwa zaidi tangu lilipoanza vuguvugu la maandamano ya upinzani katika kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi mnamo Septemba 25, ambalo lilichochewa na kile kinachojulikana kama maandamano ya Gen Z yaliyozuka katika nchi za Kenya na Nepal.