Vikosi vya Israel vyaanza kuondoka katika baadhi ya maeneo ya Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i131832-vikosi_vya_israel_vyaanza_kuondoka_katika_baadhi_ya_maeneo_ya_gaza
Vikosi vya jeshi la utawala haramu wa Israel vimeanza kuondoka katika baadhi ya maeneo Gaza baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka kupasishhwa.
(last modified 2025-10-10T11:47:40+00:00 )
Oct 10, 2025 11:47 UTC
  • Vikosi vya Israel vyaanza kuondoka katika baadhi ya maeneo ya Gaza

Vikosi vya jeshi la utawala haramu wa Israel vimeanza kuondoka katika baadhi ya maeneo Gaza baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka kupasishhwa.

Usitishaji vita unatarajiwa kuanza kutekelezwa huko Gaza, baada ya utawala ghasibu wa Israel kuidhinisha makubaliano na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS  ambayo pia yatashuhudia kuachiliwa huru mateka.

Chini ya makubaliano hayo, jeshi la Israel lina saa 24 kuondoka kwa njia iliyokubaliwa.

Hamas watakuwa na saa 72 kuwaachilia mateka wote wa Israel, wakati Israel itawaachilia mamia ya wafungwa wa Kipalestina.

Mara tu mpango huo utakapoanza kutekelezwa, malori ya misaada yataongezeka kusaidia watu milioni mbili wa Gaza, ambao wengi wao wamelazimika kuyahama makazi yao.

Inatarajiwa kuwa, ndani ya saa 72 baada ya kusainiwa makubaliano hayo, mateka 20 wa Israel na miili ya wengine 28 itaachiliwa mkabala wa kubadilishana wafungwa wapatao 2,000 wa Kipalestina, kulingana na orodha iliyotolewa na Hamas.

Wakati huo huo, kufuatia kutangazwa makubaliano ya usitishaji vita huko nchini Misri hapo jana, Hazem Qasim msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amesema kuwa, utawala wa Israel unajaribu kutumia vibaya vipengele vinavyohusiana na orodha ya wafungwa na kuondoka Gaza, na unakwepa mjadala kuhusu masuala hayo.

Amesema utawala wa Israel unajaribu kuhadaa, kufanyia hila na kuchuja baadhi ya vipengele katika makubaliano ya usitishaji vita.

Chanzo kilicho karibu na mfungwa wa Kipalestina, Marwan Barghouti mwanasiasa mashuhuri wa Palestina, kimefichua kuwa ofisi ya waziri mkuu wa Israel iliondoa jina lake kwenye orodha ya kubadilishana wafungwa dakika za mwisho, na hivyo kuhujumu makubaliano hayo ya kusitisha mapigano Gaza.