Putin: Israel imeniomba niipe Iran ujumbe kwamba haitaki vita
Rais wa Russia, Vladmir Putin amesema viongozi wa Israel wamemtaka aieleze Iran kwamba, utawala huo haufuatilii vita na makabiliano zaidi na Iran, na una hamu ya kupunguza mvutano.
Mvutano kati ya Iran na Israel ulishtadi baada ya utawala huo wa Kizayuni kuanzisha uchokozi usio na msingi dhidi ya Iran mnamo Juni 13, ambao ulichochea vita vya siku 12.
Utawala huo uliwauwa makamanda wakuu na wanasayansi wa nyuklia na pia kuua mamia ya raia kote nchini Iran. Marekani pia ilijiingiza kwenye vita hivyo na kushambulia kwa mabomu vituo vitatu vya nyuklia vya Iran katika uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Vita vya siku 12 vilimalizika Juni 24, baada ya mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran yaliyolenga maeneo ya Israel na Marekani na kuilazimisha Tel Aviv kusitisha uchokozi wake dhidi ya nchi hii.
Akihutubia mkutano wa kilele wa Asia ya Kati-Russia huko Dushanbe jana Alhamisi, Rais Putin alisema kuwa utawala wa Israel umemtaka kuwasilisha ujumbe kwa Iran.
"Tunaendelea na mawasiliano ya kujenga muamana na Israel na tunapokea ishara kutoka kwa uongozi wa Israel ukiomba kwamba hili lifikishwe kwa marafiki zetu wa Iran kwamba Israel inakusudia na imedhamiria kutatua suala hilo zaidi, na haipendezwi na aina yoyote ya makabiliano," amesema Putin.
Rais wa Russia amesisitizia ulazima wa kutatuliwa suala la nyuklia la Iran kwa njia ya mazungumzo na ndani ya fremu ya sheria za kimataifa. Amesisitizia haja ya kutafutwa suluhisho la amani kwa mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu.