Hamas yaonya; Israel inaendelea kuchuja orodha ya mateka
Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas kuushutumu utawala ghasibu wa Israel kwa 'kutia mkono' orodha ya mateka wa Kipalestina, na kukwepa kutekelezwa masharti na vipengee vya makubaliano ya usitishaji vita Gaza, licha ya ahadi zake kwa wapatanishi wa kimataifa.
Akizungumza katika mahojiano na kanali ya Al Jazeera ya Qatar, Ghazi Hamad ameonya kuwa, mwenendo huo wa utawala wa Israel unafanana na wa wapatanishi wa kimataifa wakiwemo wa Marekani.
Amebainisha kuwa, Israel inachuja orodha hiyo ya mateka na kujaribu kuondoa baadhi ya majina ya mateka wa Kipalestina wanaopasa kuachiwa huru, amesema Hamad na kuongeza kuwa, huo ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano hayo ambayo yalifikiwa kupitia upatanishi wa kimataifa.
Ameonya kuwa, baraza la mawaziri la Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu linaendelea kutishia kuanzisha tena vita dhidi ya Gaza, huku akitaka kuwepo mashinikizo ya kimataifa na ya Kiarabu ili kuizuia Israel kushambulia Gaza na kuulazimisha utawala huo utekeleze makubaliano hayo.
Kabla ya hapa, Msemaji wa Harakati ya Hamas alisema utawala wa Israel unajaribu kuhadaa, kufanyia hila na kuchuja baadhi ya vipengele katika makubaliano ya usitishaji vita.
Kufuatia kutangazwa makubaliano ya usitishaji vita huko nchini Misri hapo karibuni, Hazem Qasim amesema kuwa utawala wa Israel unajaribu kutumia vibaya vipengele vinavyohusiana na orodha ya wafungwa na kuondoka Gaza, na unakwepa mjadala kuhusu masuala hayo.
Haya yanajiri huku mchakato wa makabidhiano wa mateka wa Israel huko Gaza ukianza kutekelezwa leo kama sehemu ya makubaliano ya usitishaji vita yaliyofikiwa kati ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) na utawala wa Israel.