AU yampongeza Patrick Herminie kwa kushinda urais Ushelisheli
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131940-au_yampongeza_patrick_herminie_kwa_kushinda_urais_ushelisheli
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) Mahmoud Ali Youssouf amempongeza Patrick Herminie kwa kuchaguliwa kuwa rais mpya wa Ushelisheli.
(last modified 2025-10-13T11:09:27+00:00 )
Oct 13, 2025 10:11 UTC
  • AU yampongeza Patrick Herminie kwa kushinda urais Ushelisheli

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) Mahmoud Ali Youssouf amempongeza Patrick Herminie kwa kuchaguliwa kuwa rais mpya wa Ushelisheli.

Herminie, Spika wa zamani wa Bunge la Kitaifa la Ushelisheli alishinda duru ya pili ya uchaguzi wa urais kwa asilimia 52.7 ya kura, akimbwaga kiongozi aliyeko madarakani Wavel Ramkalawan, ambaye alipata asilimia 47.3, kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi nchini humo.

Katika taarifa yake, Youssouf amewapongeza wananchi wa Ushelisheli kwa ushiriki wao wa amani na utulivu katika kile alichokitaja kuwa ni mchakato wa kidemokrasia unaoaminika, na kuonyesha dhamira kubwa ya taifa hilo kwa utawala wa sheria na kanuni za kidemokrasia.

Aidha Youssouf amempongeza Ramkalawan na wagombea wengine kwa kukubali kushindwa na kudumisha ari ya ushindani wa kisiasa wa amani.

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Umoja wa Afrika amesisitiza dhamira ya AU ya kuisaidia Ushelisheli na kushirikiana na serikali ijayo ya nchi hiyo.

Visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi vilifanya duru ya pili ya uchaguzi wa urais kuanzia Alkhamisi hadi Jumamosi, baada ya kukosekana mgombea aliyepata kura nyingi katika duru ya kwanza ya upigaji kura uliofanyika mwishoni mwa Septemba.

Ikumbukwe kuwa, Ramkalawan aliibuka mshindi katika uchaguzi wa mwaka 2020 kwa kupata asilimia 54.9 ya kura zilizopigwa, na kumbwaga rais aliyekuwa madarakani wakati huo, Danny Faure aliyeambulia asilimia 43 ya kura.