Mkuu wa Jeshi la Wanamaji la Iran: Wamarekani wanaogopa silaha yetu mpya
-
Admiral Shahram Irani
Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kwamba majeshi ya Iran yameufunga Mlango Bahari wa Hormuz kutoka Bahari ya Arabia, akisisitiza kwamba: Adui atakutana na silaha yetu ambayo anaiogopa sana.
Admiral Shahram Irani, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema katika mahojiano maalumu ya habari kwamba katika vita vya tatu vya kulazimishwa, adui alijaribu kuikaribia Iran kutokea baharini. Ameonya kwamba: Ikiwa adui atasonga mbele zaidi, tutachukua hatua za kijeshi haraka, na tumeapa kulipiza kisasi cha mashahidi wetu hadi tone la mwisho la damu.
Admiral Irani amesisitiza kwa kusema: Karibuni sana, wataiona silaha ambayo wanaiogopa sana na iko karibu sana nao! Natarajia kwamba hawatapatwa na kiharusi!
Kamanda Irani amesema, Wamarekani ni wabaya zaidi kuliko maharamia wa Somalia, kwa sababu maharamia hao wanafanya hivyo kutokana na haja na umaskini, lakini hawa Wamarekani wamekwenda mbali hadi kwenye utekaji nyara.
Admiral Shahram Irani, ameashiria suala la kushindwa mzingiro wa baharini wa Marekani dhidi ya Iran na kusema: "Meli zimeondoka katika bandari zetu, na baadhi zimefika zilikoelekea au kutia nanga katika bandari za Iran.
Mkuu wa Jeshi la Wanamaji la Iran amesisitiza kuwa: Kama alivyoagiza Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba adui lazima apewe kipigo kikali baharini, tutahakikisha kwamba tutatoa pigo la kumfanya ajute.