UN yaonya: Hatua za Marekani zimepandisha bei ya vyakula duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i138058-un_yaonya_hatua_za_marekani_zimepandisha_bei_ya_vyakula_duniani
Msemaji wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa bei za vyakula duniani zimeongezeka kufuatia hatua za Marekani katika Mlango Bahari wa Hormuz.
(last modified 2026-04-29T10:11:50+00:00 )
Apr 29, 2026 10:07 UTC
  • Stephane Dujjaric, Msemaji wa UN
    Stephane Dujjaric, Msemaji wa UN

Msemaji wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa bei za vyakula duniani zimeongezeka kufuatia hatua za Marekani katika Mlango Bahari wa Hormuz.

Kwa mujibu wa IRNA, msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amewaambia waandishi wa habari, akinukuu data mpya kutoka kwa mashirika ya kimataifa juu ya athari mbaya za kufungwa na kuzingirwa njia ya kimkakati ya Ghuba ya Uajemi kwa bei ya bidhaa za kimsingi kwamba: "Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, "usafirishaji wa meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz umepungua kwa asilimia 95.3 tangu tarehe 28 Februari wakati Marekani na Israel zilipoanzisha vita dhidi ya Iran.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba mzingiro wa baharini umekuwa na madhara makubwa ya kiuchumi, huku "bei ya bidhaa na vyakula ikiongezeka kwa asilimia 6 na bei ya mafuta ghafi kwa soko la Ulaya imepanda kwa asilimia 53."

Stephane Dujarric pia amesema kuwa Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa UN katika Mgogoro wa Mashariki ya Kati, baada ya ziara yake ya kikanda nchini Iran, Saudi Arabia, Oman na Misri na kushiriki katika Mkutano wa Kidiplomasia wa Antalya, hivi sasa anashauriana na maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa juu ya jinsi ya kudhibiti athari mbaya za mgogoro huo.

Vita vya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimekuwa na taathira nyingi mbaya za kiusalama na kiuchumi katika maeneo mbalimbali duniani na vinaendelea kuathiri sekta tofauti za ustawi na maisha ya kila siku ya watu.