Migawanyiko yaripotiwa katika utawala wa Trump kuhusu vita dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i138038-migawanyiko_yaripotiwa_katika_utawala_wa_trump_kuhusu_vita_dhidi_ya_iran
Makamu wa Rais wa Marekani, J. D. Vance, anaripotiwa kuanza kutilia shaka kimyakimya simulizi ya matumaini inayotolewa na Wizara ya Vita ya Marekani kuhusu vita dhidi ya Iran.
(last modified 2026-04-29T11:00:42+00:00 )
Apr 29, 2026 08:59 UTC
  • JD Vance Makamu wa Rais wa Marekani
    JD Vance Makamu wa Rais wa Marekani

Makamu wa Rais wa Marekani, J. D. Vance, anaripotiwa kuanza kutilia shaka kimyakimya simulizi ya matumaini inayotolewa na Wizara ya Vita ya Marekani kuhusu vita dhidi ya Iran.

Hali hii inajiri wakati ushahidi ukiongezeka kuashiria kuwa akiba ya silaha za Marekani inapungua, ilhali uwezo wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu bado uko imara kwa kiasi kikubwa.

Maafisa waandamizi wa Marekani wanadokeza kuwa katika mikutano ya faragha, Vance amekuwa akihoji mara kwa mara namna Wizara ya Vita ya Marekani inavyowasilisha vita dhidi ya Iran, akieleza wasiwasi kuwa huenda wizara hiyo inapunguza uzito wa upungufu mkubwa wa makombora ya Marekani. Haya yameripotiwa na jarida la The Atlantic, likinukuu maafisa wawili waandamizi wa Marekani.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Vance tayari amehoji uhalali wa taarifa za kiintelijensia anazopatiwa rais, na kumwonya Rais Donald Trump kuhusu uhaba wa mifumo muhimu ya silaha.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa athari za upungufu huo ni pana, kwani akiba inayopungua inaweza kudhoofisha uwezo wa Marekani kuendeleza vita katika maeneo mengine, yakiwemo Asia ya Mashariki na Ulaya.

Wakati Waziri wa Vita Pete Hegseth pamoja na Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi Jenerali Dan Caine wakisisitiza hadharani kuwa akiba ya silaha bado iko imara na kudai Iran imepata hasara kubwa, Vance kwa upande wake ameonyesha tahadhari na mashaka yake.

Aidha, licha ya matumaini yanayoonyeshwa hadharani, taarifa za ndani za kiintelijensia zinaonyesha picha tofauti kabisa. Vyanzo vinavyofahamu tathmini za siri vinaeleza kuwa Iran bado inamiliki takribani theluthi mbili ya jeshi lake la anga, miundombinu yake mingi ya kurushia makombora, pamoja na idadi kubwa ya vyombo vya majini vya kasi vinavyoweza kufanya operesheni katika lango muhimu la bahari la Hormuz.

Marekani ikishirikiana na Israel ilianzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran Februari 28 na kuendelea kwa siku 40 kabla ya usitishaji vita. 

Katika kujibu, Jeshi la Iran lilianzisha zaidi ya mawimbi 100 ya mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyopewa jina la Operesheni Ahadi ya Kweli 4, likirusha mamia ya makombora ya balistiki na ya kasi ya juu pamoja na mashambulizi ya droni dhidi ya malengo nyeti na ya kimkakati ya Marekani na Israel kote katika eneo la Asia Magharibi.