Baadhi ya ripoti: Rais wa Madagascar ametorokea Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131962-baadhi_ya_ripoti_rais_wa_madagascar_ametorokea_ufaransa
Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa Rais Andry Rajoelina wa Madagascar ameikimbia nchi hiyo na kuelekea Ufaransa.
(last modified 2025-10-14T03:53:18+00:00 )
Oct 14, 2025 03:53 UTC
  •  Baadhi ya ripoti: Rais wa Madagascar ametorokea Ufaransa

Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa Rais Andry Rajoelina wa Madagascar ameikimbia nchi hiyo na kuelekea Ufaransa.

Vyombo vya habari vya Ufaransa vimeripoti kuwa Rais Rajoelina alisafirishwa kutoka nchini kwa ndege ya kijeshi ya Ufaransa.

Hata hivyo, taarifa rasmi kutoka serikali ya Madagascar haijathibitisha madai hayo, na hali ya sintofahamu kuhusu mahali alipo inaendelea kutanda.

Ripoti zinasema, Rais wa Madagascar Andry Rajoelina alisema ameikimbia nchi kwa kuhofia maisha yake kufuatia uasi wa kijeshi lakini hakutangaza kujiuzulu katika hotuba iliyotangazwa kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa Jumatatu kutoka eneo lisilojulikana.

Katika juhudi za kurejesha utulivu, Mkuu mpya wa majeshi, Jenerali Demosthene Pikulas, amesema kuwa jeshi na gendarmerie wanafanya kazi kwa ushirikiano kuhakikisha hali ya amani inarejea nchini.

Wiki iliyopita, Rais wa Madagascar Andry Rajoelina alimteua Ruphin Fortunat Dimbisoa Zafisambo kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo, wiki moja baada ya kuivunja serikali huku kukiwa na maandamano makubwa. Rajoelina alisema kuwa, waziri mkuu mpya lazima awe na uwezo wa kurejesha utulivu na imani ya wawananchi, kupitia kuboresha hali ya maisha na kuendeleza vipaumbele muhimu vya kitaifa.

Waandamanaji wanaoongozwa na vijana walimiminika katika Medani ya Mei 13 Jumamosi iliyopita kwa mara ya kwanza katika moja ya mikusanyiko mikubwa zaidi tangu lilipoanza vuguvugu la maandamano ya upinzani katika kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi mnamo Septemba 25, ambalo lilichochewa na kile kinachojulikana kama maandamano ya Gen Z yaliyozuka katika nchi za Kenya na Nepal.