Rais wa Madagascar akanusha taarifa kuwa ametoroka nchi
Rais Andry Rajoelina wa Madagascar amewahakikishia wananchi kwamba yeye na Waziri Mkuu wanadhibiti hali nchini humo.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa ofisi yake, Rajoelina pia alikanusha uvumi kwamba ametoroka nchi.
Katika video tofauti iliyowekwa kwenye akaunti ya Facebook, Waziri Mkuu Jenerali Rufin Zafisambo alitaka utulivu na kusihi pande zote kuweka kipaumbele kwenye mazungumzo.
"Haiwezekani kwamba vikosi vyenye silaha vinafyatuliana risasi," alisema.
Hapo awali, kulikuwa na ripoti za kurushiana risasi kati ya vitengo vya usalama vya CAPSAT na Gendarmerie kwenye kambi.
Ofisi ya Rais wa Madagascar Andry Rajoelina imesema jaribio la kunyakua mamlaka kinyume cha sheria na kinyume cha katiba linaendelea nchini humo.
Saa kadhaa baadaye, kitengo cha jeshi kinachojulikana kama CAPSAT kilidai kwamba, kilikuwa kimechukua uongozi wa kamandi ya kijeshi, na sasa kilikuwa kinadhibiti vikosi vyote vya jeshi - ardhini, angani na majini.
Hiki ndicho kitengo kile kile ambacho kilikuwa na jukumu muhimu katika mgogoro wa kisiasa wa 2009 wa Madagascar, kilichomsaidia Rajoelina kuingia madarakani.
Waandamanaji wanaoongozwa na vijana walimiminika katika Medani ya Mei 13 jana Jumamosi kwa mara ya kwanza katika moja ya mikusanyiko mikubwa zaidi tangu lilipoanza vuguvugu la maandamano ya upinzani katika kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi mnamo Septemba 25, ambalo lilichochewa na kile kinachojulikana kama maandamano ya Gen Z yaliyozuka katika nchi za Kenya na Nepal.
Maandamano ya jana Jumamosi yalikuwa makubwa zaidi kushuhudiwa katika siku kadhaa za vuguvugu lililoongozwa na vijana, ambalo lilichochewa na hasira juu ya uhaba wa umeme na maji na kuibuka kuwa kampeni pana ya kupinga serikali.