Waislamu wa Nigeria washerehekea usitishaji vita Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131928-waislamu_wa_nigeria_washerehekea_usitishaji_vita_gaza
Wanachama wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria katika Jimbo la Bauchi wamesherehekea makubaliano ya kusitisha vita Gaza, ambayo yanaruhusu maelfu ya watu kurejea kwenye nyumba zao zilizobomolewa katika ukanda wa Gaza, kuondolewa kwa vikosi vya mauaji ya halaiki ya Israel na kubadilishana mateka.
(last modified 2025-10-13T06:24:49+00:00 )
Oct 13, 2025 06:24 UTC
  • Waislamu wa Nigeria washerehekea usitishaji vita Gaza

Wanachama wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria katika Jimbo la Bauchi wamesherehekea makubaliano ya kusitisha vita Gaza, ambayo yanaruhusu maelfu ya watu kurejea kwenye nyumba zao zilizobomolewa katika ukanda wa Gaza, kuondolewa kwa vikosi vya mauaji ya halaiki ya Israel na kubadilishana mateka.

Katika mji wa Bauchi, umati wa watu ulikusanyika katika mazingira ya furaha na mshikamano, wakionyesha uungaji mkono usioyumba kwa kadhia ya Palestina. Tukio hilo liliambatana na mihadhara ya maulamaa na wasomi wa Kiislamu ambao walisisitiza umoja na haki kuwa muhimu kwa amani duniani.

Sheikh Ahmad Yusuf Yashi, mwakilishi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchhini Nigeria katika mji wa Bauchi ametoa wito wa kuwepo umoja zaidi kati ya Waislamu na Wakristo nchini Nigeria na kusisitiza kuwa, haki ya kudumu inaweza kupatikana tu kwa maelewano na mshikamano wa pande zote.

Profesa Abdullahi Danladi, mjumbe wa ngazi ya juu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na mgeni maalumu kutoka Zaria, alikaribisha usitishaji vita Gaza na kuueleza kama hatua nzuri lakini akaonya kuwa, utawala wa Kizayuni umekuwa ukikiuka mara kwa mara makubaliano ya hapo awali ya usitishaji vita.

"Amani daima inahitajika, na kila jamii yenye akili timamu inaitafuta," Danladi alisema. "Hata hivyo, historia inaonyesha kuwa, utawala wa Kizayuni hauheshimu ahadi zake. Kabla ya wino wa mikataba ya awali kukauka, walianza tena mashambulizi ya mabomu dhidi ya raia. Hivyo wakati tunasherehekea, tunaendelea kuwa waangalifu."