Mabinti barani Afrika watoa wito wa kuheshimiwa haki zao
Mabinti barani Afrika wametoa mwito wa kuheshimiwa na kupatiwa kipaumbele haki zao za kimsingi. Wito huo umetolewa katika kongamano la kieneo la mabinti magharibi mwa Afrika. Imeelezwa kuwa, haki za mabinti Afrika ni sauti ambayo haiwezi tena kupuuzwa.
Zaidi ya wasichana 100 kutoka nchi 24 za Afrika Magharibi na Kati walikusanyika katika Mkutano wa Wasichana wa Kikanda ili kueleza kwa ujasiri na kwa uwazi madai yao kwa viongozi na watunga sera chini ya mada "Haki za Wasichana haziwezi Kusubiri."
Ulimwengu ulisherehekea Siku ya Msichana wakati ambapo wasichana katika sehemu nyingi za ulimwengu hawana hali nzuri, kwa hivyo, sauti za wasichana katika sehemu nyingi za ulimwengu zimepazwa dhidi ya shida, sera mbovu, na kutojali kwa serikali.
Katika muktadha huu, sauti za wasichana kutoka nchi za Afrika Magharibi na Kati zilisikika pia kutoka Dakar, mji mkuu wa Senegal; sauti inayotaka haki, usalama, elimu, na ushiriki wa kweli katika kujenga maisha bora ya baadaye.
Wasichana wa Afrika Magharibi na Kati wanakabiliwa na changamano za kimuundo, kitamaduni na kiuchumi ambazo zinatishia maisha yao, mustakabali na haki zao za kimsingi. Ndoa za utotoni, kunyimwa elimu, unyanyasaji wa kijinsia na ukosefu wa huduma za afya za kutosha ni miongoni mwa matatizo muhimu ambayo wasichana katika sehemu hii ya Afrika wanahangaika nayo.
Wasichana kutoka Afrika Magharibi na Kati wametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kutoka kwa mamlaka za nchi mbalimbali za bara hilo ili kuboreshhwa hali zao.
Ujumbe wao, ulioelekezwa kwa marais, watunga sera, na ulimwengu, unasema: “Tunataka sauti zetu zisikike historia inapoandikwa, kwa sababu sauti zetu ni muhimu.” (Isabel kutoka Equatorial Guinea)
Wasichana wa Kiafrika siku hizi sio wahanga, bali wanaharakati waangalifu na wenye azma na dhamira ambao wanataka mustakabali sawa, salama na endelevu. Wanadai hatua madhubuti na za haraka, na sio tu kaulimbiu nzuri na tupu kwenye hafla za kimataifa.