Donald Trump, Rais wa vita
Baada ya hujuma ya hivi majuzi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, gazeti la Russia limemtaja Donald Trump kuwa "Rais wa Vita".
Tovuti ya Pars Today imelinukuu Shirika la Habari la Wanafunzi wa Iran (ISNA) na kuripoti kuwa, baada ya mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, vyombo vya habari mashuhuri vya Russia viliikosoa hatua hiyo na kumwita Donald Trump kuwa ni “Rais wa vita”. Vyombo hivyo aidha viliitaja hatua hiyo kuwa ni ishara ya mabadiliko ya kimsingi katika sera za kigeni za Marekani; mabadiliko ambayo kama inavyoamini Moscow, yanaweza kuwa na matokeo hatari kwa amani na utulivu wa kimataifa na maslahi ya kikanda ya Russia.
Vyombo vya habari vya Russia vimeripoti kuwa ndege za kivita za Marekani ziliangusha mabomu yenye uzito wa paundi 30,000 ain ya "bunker-buster" kwenye vituo vya nyuklia vya Iran katika operesheni hiyo. Shambulio hilo lilitekelezwa baada ya siku kadhaa za uvumi kuhusu iwapo Trump angeidhinisha uingiliaji wa moja kwa moja wa kijeshi wa Marekani katika vita vya Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Matukio ya hivi karibuni yameakisiwa katika magazeti kadhaa ya serikali ya Russia na yale yanayojitegemea yakiwemo magazeti ya Rossiyskaya, Komsomolskaya, Nezavisimaya Moskovsky, Komsomolets na Kommersant.
Kwa mujibu wa jarida la Newsweek, shambulio la Marekani dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya Iran litakuwa na madhara makubwa kwa maslahi ya usalama ya Marekani, masoko ya nishati ya kimataifa na eneo la Asia Magharibi.

Wakati huo huo, Rais Vladimir Putin wa Russia amelitaja shambulizi hilo kama "uchokozi usio na msingi," na vyombo vikuu vya habari vya nchi hiyo vilieleza wasiwasi wao kuhusu matokeo ya muda mrefu ya hatua hiyo kwa amani ya kimataifa na maslahi ya kieneo ya Russia.
Gazeti la "Nazavisimaya limechagua kichwa kikuu cha habari kifuatacho katika ukurasa wake wa mbele: "Trump amekuwa Rais wa vita." Gazeti hilo limeandika: "Shambulio dhidi ya Iran ni ishara ya mabadiliko ya kimsingi katika sera za kigeni za Marekani. Trump amekiuka ahadi aliyotoa katika kampeni za uchaguzi ya kuepuka vita."
Gazeti hilo pia limetahadhrisha kwamba: "Kwa Shirikisho la Russia; mabadiliko hayo katika sera ya White House si habari njema, na yanaweza kuwa na maana ya kufikia tamati jitihada za amani za Trump katika vita kati ya Russia na Ukraine."
Gazeti la serikali Rossiyskaya imeandika tena kwa dhihaka kauli mbiu ya kampeni ya Trump kwamba: “Trump ameirejesha tena Marekani vitani.”