Rais Pezeshkian: Hatusubiri maagizo au ruhusa kutoka kwa mtu yeyote
(last modified Tue, 20 May 2025 06:55:48 GMT )
May 20, 2025 06:55 UTC
  • Rais Pezeshkian: Hatusubiri maagizo au ruhusa kutoka kwa mtu yeyote

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran kamwe haisubiri maagizo au ruhusa kutoka kwa mtu yeyote na itaendelea kusimama imara kulinda haki zake kwa nguvu zake zote.

Rais Pezeshkian alisema hayo jana jioni wakati alipokutana na Bw. Fuad Hussein, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq hapa Tehran, ikiwa ni kuashiria mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani na kusisitiza kwa kusema: "Iran kamwe haitosalimu amri mbele ya mashinikizo ya kigeni. Mashinikizo hayo hayawezi kulinyima taifa letu mafanikio ya amani ya sekta ya nyuklia katika nyanja za afya, matibabu, kilimo na viwanda. Hatusubiri amri wala ruhusa kutoka kwa mtu yeyote kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya taifa letu."

Akizungumzia uhusiano wa kina na wa kihistoria kati ya mataifa haya mawili ya Iran na Iraq, Rais Pezeshkian amesema: "Uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq haukuanza jana na leo, bali unatokana na misingi iliyokita mizizi ya miaka elfu moja iliyopita."

Usawa wa makabila ya Iran na Iraq, usawa wa lugha na utamaduni kati ya watu wa pande zote za mipakani, kuwa na mpaka mrefu wa pamoja, yote hayo yanaonesha kwamba uhusiano wa mataifa mawili ya Iran na Iraq hauwezi kabisa kuvunjika na hayo yote yanaonesha wazi kina kirefu cha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ndugu.

Akisisitiza utayari wa Iran wa kuzinufaisha nchi nyingine za Kiislamu na majirani zake kutokana na uzoefu na mafanikio yake katika nyanja mbalimbali ikiwemo matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwenye sekta za dawa, kilimo na viwanda, Rais Pezeshkian amesema: "Milango ya maingiliano na ushirikiano kati yetu na serikali ya Iraq iko wazi kwenye nyuga zote. Tunayahesabu maendeleo ya Iraq kuwa ni maendeleo yetu, na maendeleo ya Iran kuwa ni maendeleo ya Iraq.

Kwa upande wake, Bwana Fuad Hussein, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq ameelezea kufurahishwa kwake na mazungumzo yake hayo ya ana kwa ana na Rais Pezeshkian na kusema,  "Uhusiano wa Iraq na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uko katika kiwango kizuri na chenye nguvu. Maingiliano ya kibiashara na kiuchumi kati ya nchi hizi mbili yamepanuka na yanazidi kustawi."