Hatimaye Sudan yapata Waziri Mkuu mpya
Kiongozi wa Kijeshi wa Sudan Abdel Fattah al-Burhan amemteua Kamil El-Tayeb Idris Abdelhafiz kuwa waziri mkuu mpya wa taifa hilo, ikiwa ni miaka miwili tangu vita kuzuka nchini humo.
Kamil Idris, ni mwanadiplomasia wa kutajika, aliwahi pia kuhudumu kama mkurugenzi mkuu wa shirika la umoja wa mataifa la haki miliki, WIPO, lakini pia alihudumu katika ujumbe a kudumu wa Sudan katika umoja wa mataifa.
Mwaka wa 2010, Kamil aliwania urais dhidi ya Omar al-Bashir na uteuzi wake unajiri wakati huu wapiganaji wa RSF wakiendelea mashambulio yao katika miji mbalimbali nchini humo.
Idris anachukua nafasi ya mwanadiplomasia mkongwe Dafallah al-Haj Ali, ambaye aliteuliwa na Burhan mwishoni mwa mwezi Aprili na kuhudumu chini ya wiki tatu kama kaimu waziri mkuu.
Awali Burhan alidokeza kuhusu kuunda serikali ya kipindi cha vita kwa lengo la kuikomboa Sudan kutoka kwa waasi.
Wakati huo huo, jeshi la Sudan limefanikiwa kutwaa tena udhibiti wa eneo muhimu la kistratajia la Attrun huko Darfur Kaskazini kutoka kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

"Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya Pamoja vimepata ushindi mkubwa kwa kukomboa eneo la kimkakati la Attrun kutoka mikononi mwa wanamgambo wa kigaidi wa RSF," Gavana wa Darfur, Minni Arko Minnawi amesema katika ujumbe wake aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.
Mgogoro wa takriban miaka miwili kati ya SAF na RSF umesababisha makumi ya maelfu ya watu kuuawa, kuwa wakimbizi zaidi ya watu milioni 15, na kuisukuma Sudan kwenye ukingo wa janga la njaa. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa.
Vita hivyo vimeporomosha kabisa mfumo wa huduma ya afya nchini Sudan huku takwimu za majeruhi zikiendelea kuwa ngumu kujulikanana kutokana na mazingira mabaya na tata ya vita.
Juhudi za kupatanisha na kuleta usitishaji mapigano zimekwama, huku pande zote mbili zikishutumiwa kukiuka haki za binadamu na kuzuia misaada ya kibinadamu.