Pezeshkian: Iran inafanya mazungumzo, lakini haigopi vitisho vyovyote
Rais Masoud Pezeshkian amesisitiza kuwa, Iran haitasalimu amri na kuachana na haki zake licha ya vitisho, akieleza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitaachana na mafanikio yake ya heshima katika nyanja yoyote ile, iwe kisayansi au kijeshi.
Akizungumza leo Jumamosi, Rais wa Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haitakubali vitisho au kuacha mafanikio yake katika sekta zote. "Hatutakubali uonevu na kuburuzwa," amesisitiza Rais Pezeshkian.
Ameeleza bayana kwamba, katika hali ambayo wanasayansi wa Iran wanauawa, lakini Iran yenyewe inatuhumiwa kwa ugaidi na magaidi halisi. "Sisi ni waathirika wa ugaidi," ameongeza Dakta Pezeshkian na kueleza kuwa, "Kwa sababu Iran inakataa kupigishwa magoti, inaitwa 'chanzo cha ukosefu wa usalama katika eneo."
Pezeshkian amesema maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanajaribu kuisawiri Iran kuwa inaandamwa na udhaifu na migawanyiko, lakini uhalisia ni kuwa maendeleo ya Wairani katika sekta mbalimbali yanawakatisha tamaa.
Kuhusu matamshi ya hivi majuzi ya Rais wa Marekani, Donald Trump wakati wa ziara yake katika mataifa ya Ghuba ya Uajemi, Rais wa Iran amesema kuwa, hakuna mtu anayeweza kuamini kauli za Trump dhidi ya Iran isipokuwa Trump mwenyewe.
Amesema Trump anazungumza juu ya amani na utulivu, na wakati huo huo anatishia kutumia silaha za maangamizi makubwa, akiwasilisha ujumbe wa kinzani wa 'amani' na 'mauaji.'
Pezeshkian pia amesema kuwa Iran haitafuti vita, na kwamba licha ya Wairani kutaka mazungumzo, lakini kamwe hawatababaishwa na vitisho, na pia hawawezi kuachana na haki zao za kisheria.
Hali kadhalika amewakosoa wale wanaodai kuunga mkono haki za binadamu huku wakikaa kimya kuhusu mauaji ya karibu Wapalestina 60,000 wasio na ulinzi yaliyofanywa na utawala wa Israel Gaza. "Hawapaswi kuzungumzia amani na haki za binadamu baada ya (kufanyika) mauaji ya watu wasio na hatia (Gaza)," amesema.