Rafael Grossi: Iran haina silaha za nyuklia
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amesema kuwa suluhisho la muda mrefu la suala la nyuklia la Iran ni mazungumzo ya kidiplomasia, akisisitiza kuwa Iran haina silaha za nyuklia.
Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, ambaye hapo awali alifungua njia ya uchokozi wa Marekani na Wazayuni dhidi ya Iran kwa kutoa azimio dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Tehran, amesema katika mahojiano maalumu ya kipindi cha CBS cha "Face the Nation" kwamba: "Uwezo wa nyuklia wa Iran na ujuzi wa kiufundi wa Jamhuri ya Kiislamu bado uko palepale na suluhisho pekee la muda mrefu ni mazungumzo ya kidiplomasia."
Grossi ameongeza kuwa: "Tunafanya mawasiliano ya mara kwa mara, sasa mawasiliano yanapaswa kuanzishwa upya."
Grossi, amekiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba hakukuwa na uharibifu mkubwa kwa vifaa vya nyuklia vya Iran baada ya shambulizi la Marekani, na kudai kuwa: "Ninaamini Wairani wanaweza kuanza kutumia mashinepewa (centrifuge) zenye uwezo wa kuzalisha uranium iliyorutubishwa ndani ya miezi michache au chini ya muda huo."
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, katika kikao cha hadhara cha Jumatano iliyopita, Julai 25, wawakilishi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) walipasisha muswada wa kusitisha ushirikiano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kwa kura 210 za ndio, kura 2 za kupinga, na 2 za waliojizuia kupiga kura kati ya wabunge 219 waliohudhuria kikako hicho.
Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi, Ijumaa, Julai 27, aliandika katika mtandao wa kijamii wa "X" kwamba azimio la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu la kusimamisha ushirikiano na IAEA ni "matokeo ya moja kwa moja ya nafasi ya kusikitisha ya Rafael Grossi" na akasema: "Hatua za kiupendeleo za Grossi pia zilifungua njia moja kwa moja ya Baraza la Magava la IAEA kupasisha muswada wenye malengo ya kisiasa dhidi ya Iran na kuwezesha mashambulizi haramu ya Israel na Marekani kwenye vituo vya nyuklia vya Iran."