Utoshelevu wa chakula; Afrika yatakiwa iongeze bajeti kwenye kilimo
Serikali za nchi za Afrika zimehimizwa kuongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo ili kuimarisha usalama wa chakula na kufungua mustakbali wa maendeleo endelevu ya kiuchumi.
Wito huo umetolewa na washiriki wa mkutano wa kilele kuhusu uwekezaji endelevu kwenye mifumo ya kilimo na chakula, uliowaleta pamoja watungaji sera na wadau wa kilimo, kuchunguza mbinu za ufadhili kwa lengo la kuleta mabadiliko katika mifumo ya chakula kote barani Afrika.
Katika mkutano huo wa siku tatu uliofanyika Nairobi, mji mkuu wa Kenya, wajumbe wamesema ingawa sekta ya kilimo inaajiri asilimia 60 ya watu barani Afrika, lakini bado sekta hiyo inaendelea kupata uwekezaji mdogo kuliko inavyohitajika.
Waziri wa Kilimo na Ustawishaji wa Mifugo wa Kenya, Mutahi Kagwe amesema sekta ya kilimo inapokea asilimia 3 tu ya bajeti ya taifa licha ya mchango wake wa asilimia 22.5 kwa Pato Ghafi la Taifa GDP.
Waziri huyu amesema kunyanyua kiwango cha uwekezaji hadi asilimia 10 ya bajeti ya taifa, kutaongeza tija ya uzalishaji kwa asilimia 45, kutokomeza hasara za baada ya mavuno, na kuongeza mara tatu biashara ya mazao ya kilimo ndani ya Afrika kufikia mwaka 2035.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Afrika Mashariki (IGAD), watu milioni 67.4 wa eneo la Pembe ya Afrika hawana uhakika wa chakula.
Nairobi inatazamiwa kuwa mwenyeji wa Kongamano na Maonyesho ya 10 ya Kimataifa ya Kilimo Afrika (Agritec Africa 2025) kuanzia Juni 11 hadi 13 katika Jumba la Kimataifa la Mikutano la Kenyatta (KICC) jijini Nairobi.