Spika Qalibaf: Iran, Algeria zinahitaji kufanya kazi kusaidia usambazaji wa misaada Gaza
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf amesema Iran na Algeria zinahitaji kufanya kazi ili kusaidia juhudi za kufikisha misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza uliokumbwa na vita.
Qalibaf ameyasema hayo katika kikao chake na Spika wa Bunge la Watu wa Algeria, Ibrahim Boughali, katika mji mkuu wa Indonesia, Jakarta, kando ya Mkutano wa 19 wa Umoja wa Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (PUIC).
Amesisitiza umuhimu wa kuwepo umoja na mshikamano mbele ya mshambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel huko Palestina na kurejesha haki za wananchi madhulumu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
Spika wa Bunge la Iran amekosoa ukosefu wa umoja baina ya nchi za Kiislamu katika kuiunga mkono Palestina na kusema: "Hii leo sio tu kwamba baadhi ya nchi za Kiislamu haziwasaidii Wapalestina, bali pia baadhi ya nchi hizo zinawaunga mkono Wazayuni katika mazingira hayo ya kidhalimu."
Qalibaf amezitaka nchi za Kiislamu kutafuta suluhisho la mgogoro huo na kutoa wito kwa mataifa mengine kuendelea kuifahamu ipasavyo kadhia ya mapambano ya Palestina ili kulisaidia taifa hilo kupata ushindi wa mwisho.
Vilevile ameyataka mabunge ya nchi za Kiislamu kuwa na misimamo ya wazi kuhusu suala la Palestina.

Wapalestina zaidi ya elfu 52 wameuawa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na wengine 119,846 wamejeruhiwa katika hujuma na mashambulizi ya kikatili ya jeshi la Israel huko Gaza tangu Oktoba 7, 2023.